
Rais William Ruto ameendelea kufanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri kwa mara nyingine, akiwahamisha mawaziri wawili, kumteua waziri mpya, na kumfuta mmoja.
Katika mabadiliko ya hivi punde yaliyotangazwa Jumatano, Machi 26, Ruto alimuondoa Justin B. Muturi kutoka Wizara ya Utumishi wa Umma, Maendeleo ya Rasilimali Watu na Masuala Maalum na kumkabidhi wadhifa huo Mbunge wa Mbeere Kaskazini, Geoffrey K. Kiringa Ruku.
Aden Duale, aliyekuwa Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, amehamishiwa Wizara ya Afya, ambayo hapo awali ilikuwa chini ya Dkt. Deborah Mlongo Barasa. Dkt. Barasa sasa atachukua nafasi ya Duale katika Wizara ya Mazingira.
Aidha, Bi. Hanna Wendot Cheptumo amependekezwa kujiunga na Baraza la Mawaziri kama Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi, lakini uteuzi wake unahitaji kuidhinishwa na Bunge.
"Kwa hatua hii ya Rais, Baraza la Mawaziri litafikia
idadi yake kamili kikatiba, jambo litakaloongeza uwezo wa Serikali kuendelea
kusukuma mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini. Ikiwa watateuliwa na Bunge,
mawaziri hawa watajiunga na chombo kikuu cha kutunga sera nchini kama Mawaziri
wa Baraza la Mawaziri," ilisomeka taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Utumishi
wa Umma na Katibu Mkuu wa Ikulu, Felix Koskei.
Mabadiliko ya hivi punde katika Baraza la Mawaziri yanakuja siku moja baada ya Rais William Ruto kumshutumu hadharani aliyekuwa Justin Muturi, kwa kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali..
Akizungumza katika hafla ya futari Ikulu mnamo Machi 25, 2025, Rais Ruto alimlaumu Muturi kwa kuchelewesha uanzishwaji wa Mfuko wa Waqf wa Kiislamu, akidai kuwa ufanisi wake ulikuwa wa kiwango cha chini alipokuwa Mwanasheria Mkuu.
"Nilikuwa na tatizo na Mwanasheria Mkuu aliyekuwepo hapo awali—alikuwa hana uwezo. Lakini sasa, nina mtu mwenye uwezo mkubwa katika nafasi hiyo, na nina hakika masuala ya Waqf yatatatuliwa ndani ya miezi michache," alisema Ruto.
Muturi hakusita kujibu tuhuma hizo, akisema kuwa madai ya Ruto
hayakuwa ya kweli. Alieleza kuwa Sheria ya Waqf Na. 8 ya 2022 haielekezi
kuanzishwa kwa "Mfuko wa Waqf wa Kiislamu" na kuongeza kuwa waqf ni
mali ya hisani inayosimamiwa na Tume ya Waqf.