
Kuna hisisa za Ghadhabu nchini Somalia baada ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane, ambaye alikuwa ametoweka kwa miezi sita, kupatikana akiishi na mwanamume aliyesema kuwa ni mumewe.
Msichana huyo aliripotiwa kutoweka na familia yake katika eneo lililojitangazia uhuru wake la Puntland Septemba mwaka jana.
Miezi kadhaa baadaye, taarifa ziliibuka kuwa baba yake msichana huyo aliruhusu mtoto huyo aolewe na mtu mzima aliyeitwa Sheikh Mahmoud.
Vikosi vya usalama viliizingira nyumba ya mwanamume huyo wiki iliyopita na kulazimisha kuingia ndani baada ya kujifungia chumbani na msichana huyo.
Tukio hilo limezua hasira kwenye mitandao ya kijamii na maandamano ya umma katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Pia imeibua mijadala mipya kuhusu sheria za ulinzi wa mtoto, kwani kwa sasa hakuna umri wa chini kabisa wa kisheria wa kuolewa.
"Kinachoshangaza zaidi kuliko mkasa wenyewe ni madai ya kutekwa nyara na ukweli kwamba familia yake haikuwa na habari kuhusu aliko kwa miezi kadhaa," Fadumo Ahmed, mwenyekiti wa kundi linaloongoza la kutetea haki za wanawake wa Somalia, aliiambia BBC.
"Tunaamini taasisi zinazohusika kuchukua hatua za kisheria zinazofaa na zinazohitajika."
Kulingana na mjomba wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka minane, alichukuliwa kutoka nyumbani kwake katika jiji la Bosaso Septemba iliyopita na jamaa wa kike. Jamaa huyu alisema alikuwa akimsindikiza mtoto huyo safarini kwenda kuonana na mjomba mwingine.
Lakini miezi kadhaa baadaye, video iliibuka mtandaoni, ikimuonyesha msichana huyo akisoma Quran.
Familia yake baadaye ilianzisha utafutaji wa mtoto - haijulikani kwa nini hawakufanya hivi mapema.
Waligundua alikuwa katika eneo la Carmo, akiishi na Sheikh Mahmoud.
Sheikh Mahmoud awali alisema alikuwa akimfundisha msichana huyo Quran pekee. Lakini baada ya malalamiko ya kisheria kuwasilishwa, alibadilisha kauli yake, akisema alimuoa msichana huyo kwa idhini ya baba yake.
Alipoulizwa na BBC jinsi alivyohalalisha kuoa mtoto wa miaka minane, Sheikh Mahmoud alisema kwamba tamaduni za Mtume wa Uislamu Muhammad, pamoja na zile za Shafi'i, ziliruhusu ndoa za utotoni.
Baada ya BBC kuhoji hoja yake - ikitoa upinzani kutoka kwa wasomi wengi wa Kiislamu wa Somalia - Sheikh Mahmoud alishikilia kuwa hataiacha ndoa hiyo.