logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wasiwasi huku genge likivamia msafara wa MSS nchini Haiti, polisi mmoja wa Kenya hajulikani aliko

Kufuatia mashambulizi hayo, afisa mmoja wa Kenya anayehudumu chini ya MSS bado hajapatikana.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri26 March 2025 - 07:45

Muhtasari


  • Juhudi za kuwaokoa maafisa wa Haiti zilitatizika baada ya moja ya magari ya MSS pia kukwama, huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi.
  • MSS imeahidi kutoa taarifa ya kina baadaye kuhusu tukio hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa maafisa wake.
Kenyan police officers arriving in Haiti

Afisa mmoja wa Kikosi cha Kenya kinachohudumu chini ya Mpango wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa (MSS) hajulikani aliko baada ya shambulio lililotekelezwa na magenge ya uhalifu nchini Haiti.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, Machi 25, 2025, na msemaji wa MSS, Jack Ombaka, shambulio hilo lilitokea mnamo saa nne unusu jioni katika eneo la Pont-Sonde, jimbo la Artibonite, wakati gari la kivita la Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) lilipokwama kwenye mtaro unaoshukiwa kuchimbwa kwa makusudi na magenge ya wahalifu.

“Tulipopokea taarifa za tukio hilo, magari mawili ya kivita ya MSS Mine-Resistant Ambush Protected (MRAP) yalitumwa kutoka Pont-Sonde kusaidia katika operesheni ya uokoaji,” taarifa hiyo ilieleza.

Hata hivyo, juhudi za kuwaokoa maafisa wa Haiti zilitatizika baada ya moja ya magari ya MSS pia kukwama, huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi. Wakati vikosi vya uokoaji vikiendelea kushughulikia hali hiyo, washukiwa wa magenge waliokuwa wamejificha walitekeleza shambulio la kushtukiza.

Kufuatia mashambulizi hayo, afisa mmoja wa Kenya anayehudumu chini ya MSS bado hajapatikana. Ombaka alisema vikosi maalum vimeanzisha msako ili kubaini aliko.

“Kufuatia tukio hili, afisa mmoja wa Kikosi cha Kenya hajulikani aliko. Timu maalum za utafutaji na uokoaji zimepelekwa kufuatilia nyayo zake na kubaini alipo,” alisema msemaji wa MSS, Jack Ombaka.

MSS imeahidi kutoa taarifa ya kina baadaye kuhusu tukio hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti.

Kenya ilituma maafisa wake wa polisi nchini Haiti kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kurejesha utulivu katika taifa hilo la Karibea, ambalo linakabiliwa na ongezeko la mashambulio kutoka kwa magenge ya wahalifu.

Mwezi uliopita, Afisa mmoja wa polisi kutoka Kenya aliyekuwa amejitolea kusaidia kurejesha utulivu nchini Haiti alipoteza maisha baada ya kushambuliwa kwa risasi wakati wa operesheni katika eneo la Artibonite.

Tukio hilo lilitokea wakati maafisa walipokuwa wakijibu mwito wa dharura kutoka kwa wakazi wa Pont-Sondé, sehemu inayokumbwa na mashambulizi ya magenge.

Licha ya juhudi za kumwokoa kwa kumpeleka hospitalini kwa njia ya anga, afisa huyo alifariki kutokana na majeraha yake.

Kamanda wa Kikosi Cha Usalama cha Kimataifa kinachosaidia katika operesheni ya kulinda amani Haiti, Godfrey Otunge, alisema afisa huyo alisafirishwa kwa ndege hadi katika Hospitali ya Level Two ya Aspen ambako alifariki kutokana na majeraha.

“Mnamo Februari 23, 2025, mmoja wa afisa wetu wa MSS kutoka kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni huko Segur-Savien katika idara ya Artibonite. Afisa huyo alisafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Aspen Level 2 lakini, kwa bahati mbaya, alifariki kutokana na majeraha,” akasema kwenye taarifa.

Hili lilikuwa ni tukio la kwanza la vifo miongoni mwa maafisa wa kikosi cha kimataifa kinacholenga kurejesha usalama nchini Haiti.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved