

Afisa mmoja wa polisi kutoka Kenya aliyekuwa amejitolea kusaidia
kurejesha utulivu nchini Haiti alipoteza maisha yake siku ya Jumapili baada ya
kushambuliwa kwa risasi wakati wa operesheni katika eneo la Artibonite.
Tukio hilo lilitokea wakati maafisa walipokuwa wakijibu mwito wa dharura kutoka kwa wakazi wa Pont-Sondé, sehemu inayokumbwa na mashambulizi ya magenge.
Licha ya juhudi za kumwokoa kwa kumpeleka hospitalini kwa njia ya anga, afisa huyo alifariki kutokana na majeraha yake.
Kamanda wa Kikosi Cha Usalama cha Kimataifa kinachosaidia katika operesheni ya kulinda amani Haiti, Godfrey Otunge, alisema afisa huyo alisafirishwa kwa ndege hadi katika Hospitali ya Level Two ya Aspen ambako alifariki kutokana na majeraha.
“Mnamo Februari 23, 2025, mmoja wa afisa wetu wa MSS kutoka kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni huko Segur-Savien katika idara ya Artibonite. Afisa huyo alisafirishwa kwa ndege hadi Hospitali ya Aspen Level 2 lakini, kwa bahati mbaya, alifariki kutokana na majeraha,” akasema kwenye taarifa.
Hili ni tukio la kwanza la vifo miongoni mwa maafisa wa kikosi cha kimataifa kinacholenga kurejesha usalama nchini Haiti.
Afisa huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha polisi wa Kenya wapatao 800 waliotumwa Haiti kusaidia Jeshi la Polisi la Taifa la Haiti.
Mnamo Februari 2025, kundi jingine la maafisa 217 lilijiunga na wenzao waliokuwa tayari wameanza kazi, wakifanya kazi kwa pamoja na vikosi kutoka mataifa mengine kama vile Jamaica, Guatemala, na El Salvador.
Lengo kuu la operesheni hiyo ni kupambana na ongezeko la uhalifu wa magenge ambayo yameimarika tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mwaka 2021.
Eneo la Artibonite, hususan Pont-Sondé, limeathiriwa pakubwa na magenge kama Gran Grif, ambayo yamekuwa yakitumia hali ya kisiasa iliyojaa machafuko kupanua mamlaka yao.
Habari za kifo cha afisa huyo zimeibua simanzi kubwa kwa jamii ya kimataifa na kwa wakazi wa Haiti.
Kamanda wa vikosi vya Kenya nchini Haiti, Godfrey Otunge, alieleza huzuni yake akisema, "Afisa huyu alitoa maisha yake kwa ajili ya watu wa Haiti, akipambana kuhakikisha usalama wao."
Viongozi wa operesheni hiyo walitoa shukrani kwa madaktari na maafisa wa jeshi la El Salvador kwa juhudi zao za haraka baada ya tukio hilo. Huko Kenya, Jeshi la Polisi la Taifa lilitoa rambirambi kwa familia ya marehemu na kumuenzi afisa huyo kwa ujasiri wake na kujitolea kwa amani ya kimataifa.
Kifo hiki kimezua mjadala kuhusu usalama wa maafisa wa Kenya wanaopelekwa katika maeneo yenye machafuko.
Wadau mbalimbali wanatoa wito wa tathmini ya kina kuhusu hatua za usalama ili kuhakikisha kuwa maafisa hao wanapewa ulinzi wa kutosha wanaposhiriki operesheni hatari kama hizi.
Hali nchini Haiti inazidi kuwa ya wasiwasi, huku jamii ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu ili kuona juhudi zaidi za kusaidia kurejesha utulivu. Kifo cha afisa huyu wa Kenya kinabaki kuwa kumbukumbu ya hatari wanazokabiliana nazo wale wanaojitolea kupambana na uhalifu na kurejesha amani katika maeneo yaliyoathirika na ghasia.