
WAZIRI wa Elimu, Julius Ogamba Migos amewanyooshea wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Butere kidole cha lawama kwa kukataa kuonyesha maigizo yao licha ya kupewa fursa ya kupanda jukwaani.
Akizungumza katika kaunti ya Nakuru adhuhuri
ya Alhamisi kufuatia tukio hilo ambalo limeacha taifa katika gumzo kubwa,
Ogamba alisema kwamba wanafunzi hao walikataa wenyewe kuonyesha igizo lao la ‘Echoes
of War’ licha ya kukubaliwa na hata kuitwa kupanda jukwaani.
Kwa mujibu wa Waziri Ogamba, wanafunzi hao
walipewa fursa ya kupanda jukwaani majira ya saa mbili asubuhi ya Alhamisi ili
kutoa onyesho lao, lakini baada ya kufika jukwaani, waliimba wimbo wa taifa na
kuondoka.
CS Ogamba alieleza kwamba mmoja wa wanafunzi
hao alijongea mbele baada ya kuimba wimbo wa taifa na kusema kwamba hawangeweza
kuonyesha igizo lao bila ya kuwepo kwa mkurugenzi wao, Cleophas Malala.
Ogamba hata hivyo alihoji Malala alikuwa na
umuhimu gani wa kuwepo katika ukumbi ili igizo hilo kuendelea, akisema kwamba
yeye si Mwalimu wala mkurugenzi katika shule ya Butere Girls.
“Tuna ufahamu wa kutosha kwamba
wanafunzi walipewa fursa ya kuonyesha mchezo wao majira ya saa mbili asubuhi. Wakati
walifika ukumbini na baada ya kuimba wimbo wa taifa, mmoja wao alijongea mbele
na kusema kwamba hawako tayari kucheza igizo lao bila ya mkurugenzi wao, bwana
Malala.”
“Na Bwana Malala si Mwalimu katika shule ya Butere, yeye si mkurugenzi katika shule ya Butere na hata si muongozaji wa igizo hilo. Hivyo wanafunzi kwa hiari yao tu walisema hawawezi kuonyesha mchezo wao,” Ogamba alisisitiza.
Kuhusu suala la vurugu kutoka kwa polisi
ambao wanasemekana kutupa vitoza machozi katika shule walimofanya makaazi yao
ya muda wasichana wa Butere, Ogamba alisema kwamba hana Habari kuhusu hilo huku
akiahidi kutoa taarifa baada ya kuarifiwa na mamlaka husika.
Mchezo wa kuigiza wa ‘Echoes of War’ ambao
uliandikwa na aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala umekuwa gumzo katika
siku za hivi karibuni haswa baada ya kupigwa marufuku na kusababisha suala hilo
kuishia mahakamani.
Mahakama ilitoa uamuzi wa mchezo huo wa
kuigizwa kuendelea bila kuhitilafiwa na yeyote, lakini siku moja kabla ya siku
ya maonyesho katika kaunti ya Nakuru, vurumai zilizuka, Malala akiripotiwa
kuzuia kuingia katika eneo walimokuwa wanafunzi hao.