
Papa Francis anatibiwa kutokana na kwamba hayuko katika "hali nzuri kiafya" na atasilia hospitalini kadiri na kutakavyokuwa na ulazima wa kufanya hivyo, Vatican imesema.
Papa mwenye umri wa miaka 88 alilazwa katika Hospitali ya Gemelli huko Roma siku ya Ijumaa ili kupata matibabu na kufanyiwa vipimo vya matatizo ya kupumua.
Katika taarifa zilizotolewa siku ya Jumatatu, Vatikani ilisema Papa ana "maambukizi yanayosababishwa na mchanganyiko wa virusi, bakteria na vimelea" katika njia yake ya kupumua, ambayo yanahitaji matibabu mengine.
Kabla ya kulazwa wiki iliyopita, Papa alikuwa na dalili za ugonjwa wa kupumua kwa siku kadhaa na alikuwa amewakabidhi maafisa kusoma hotuba zilizoandaliwa kwenye hafla.
Msemaji wa Vatican Matteo Bruni aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba Papa alikuwa katika hali nzuri.
Taarifa fupi kuhusu hali yake ilisema: "Vipimo vyote vilivyofanywa hadi sasa vinaonyesha hali yake sio ya kuridhisha na itahitaji alazwe hospitalini kupata matibabu mwafaka."
Hadhira ya maombi ya kila wiki ya Papa - ambayo kawaida hufanyika kila Jumatano - imeahirishwa kwa wiki hii, taarifa hiyo iliongeza.
Taarifa zaidi kuhusu hali ya Papa itatolewa baadaye Jumatatu, Bw Bruni aliongeza.
Papa mwenye asili ya Argentina ametumia karibu miaka 12 kama kiongozi wa Kanisa Katoliki la Roma.
Mnamo mwezi Machi 2023, aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo hiyo kwa siku tatu na kupata matibabu ya matatizo kupumua.
Mnamo Desemba mwaka huo huo, alilazimika kukatisha safari yake ya kwenda Falme za Kiarabu kwa mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 kwa sababu ya ugonjwa mwingine.
Amekuwa akikabiliwa na matatizo kadhaa ya kiafya katika maisha
yake yote, ikiwa ni pamoja na kuondolewa sehemu ya pafu lake akiwa na umri wa
miaka 21.