logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Utata huku tiktoker akifungwa jela kwa kumwagiza Yesu anyoe nywele zake

Mtumiaji huyo wa tiktok alimwambia Yesu kupitia picha kwenye simu yake kwamba anapaswa kunyoa nywele.

image
na Samuel Mainajournalist

Kimataifa11 March 2025 - 12:05

Muhtasari


  • Kauli ya Ratu ilizua ghadhabu kali miongoni mwa Wakristo, huku makundi kadhaa ya kidini yakifungua malalamiko rasmi dhidi yake.
  •  Mahakama ilimhukumu Ratu kifungo cha miaka miwili na miezi kumi kwa kosa la kukashifu dini.

sheria mahakamani

Mahakama moja nchini Indonesia imemhukumu Ratu Thalisa, maarufu kama Ratu Entok, kifungo cha miaka miwili na miezi kumi kwa kosa la kukashifu dini. Hii ni baada ya mtumiaji huyo wa tiktok kumwambia Yesu kupitia picha kwenye simu yake kwamba anapaswa kunyoa nywele..

Thalisa, mwanamke aliyebadili jinsia (transgender) na Mwislamu mwenye zaidi ya wafuasi 442,000 kwenye TikTok, alikuwa akiendesha kipindi cha moja kwa moja alipokumbana na ujumbe kutoka kwa mmoja wa watazamaji wake akimshauri akate nywele zake ili aonekane wa kiume zaidi.

Huku akijibu, alishika simu yake, akaonyesha picha ya Yesu na kusema: "Yesu, tafadhali nenda ukanyoe nywele zako."

Kauli hiyo ilizua ghadhabu kali miongoni mwa Wakristo nchini Indonesia, huku makundi kadhaa ya kidini yakifungua malalamiko rasmi dhidi yake kwa kosa la kukashifu dini (blasphemy).

Mahakama ya Medan, Kaskazini mwa Sumatra, ilisema matamshi ya Thalisa yalihatarisha utulivu wa umma na maelewano ya kidini, hivyo ilimhukumu kifungo cha miaka miwili na miezi kumi jela.

"Mshtakiwa alitumia jukwaa la mitandao ya kijamii kwa njia inayoweza kuvuruga amani ya umma na mshikamano wa kidini," ilisema mahakama katika uamuzi wake.

Hukumu hiyo ilikuja baada ya mashirika kadhaa ya Kikristo nchini humo kufungua malalamiko rasmi kwa polisi wakidai kuwa kauli ya Thalisa ilikuwa ya dharau kwa Ukristo.

Hukumu hiyo imekosolewa vikali na mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International, ambalo lilielezea hukumu hiyo kama shambulio la kushangaza dhidi ya uhuru wa kujieleza wa Ratu Thalisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International Indonesia, Usman Hamid, alisema serikali inatumia sheria vibaya kuwakandamiza watu kwa maoni yao mitandaoni.

"Mamlaka za Indonesia hazipaswi kutumia sheria ya EIT kuwaadhibu watu kwa maoni yao mitandaoni," alisema Hamid, akiongeza kuwa matamshi ya Thalisa hayakufikia kiwango cha uchochezi wa chuki za kidini.

Sheria ya Electronic Information and Transactions (EIT) ilianzishwa mwaka 2008 na kurekebishwa mwaka 2016 kwa lengo la kulinda watu dhidi ya kashfa na taarifa za uongo mitandaoni. Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wameeleza wasiwasi wao kwamba sheria hiyo inatumiwa kudhibiti uhuru wa maoni.

Ripoti ya Amnesty International inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2019 na 2024, watu 560 walifunguliwa mashtaka chini ya sheria hii kwa maoni yao mitandaoni, huku 421 wakihukumiwa.

"Sheria hii ina vipengele vinavyonyima watu haki yao ya kujieleza kwa uhuru," alisema Hamid, akitoa wito kwa serikali ya Indonesia kufanya marekebisho makubwa katika sheria hiyo.

Kesi ya Ratu Thalisa imeibua mjadala mkubwa kuhusu uwiano kati ya uhuru wa kujieleza na heshima kwa imani za kidini nchini Indonesia.

Wakati baadhi ya watu wanaona hukumu yake kama haki kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo, wengine wanahoji ikiwa serikali inatumia sheria hizi kuwakandamiza wachache, wakiwemo watu wa jamii ya LGBTQ+ na wanaharakati wa haki za binadamu.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved