
BUNGE wa Mumias Mashariki, Peter Salasya ameonesha furaha yake baada ya ukurasa wake wa mitandao wa video fupi wa TikTok kufikisha wafuasi zaidi ya laki nane wikendi ilityopita.
Mbunge huyo anayejiweka kifua mbele kama mtetezi wa sera za
vijana wa Gen Z alichukua kwenye ukurasa wake Facebook na kuwashukuru mashabiki
wake 800k kwenye TikTok huku akisema kwamba Mungu ana sababu ya kumfanya yeye
kuwa na ufuasi huo.
“Mimi sasa ndiye
mwanasiasa anayeongoza katika kuwa na wafuasi wengi kwenye TikTok nchini Kenya.
Kufikisha wafuasi 801400 kwenye tiktok na wewe ni mwanasiasa sio utani. Nataka
kuwashukuru wakenya wote wanaofuata. Mungu ana sababu kwanini amenipa ufuasi
huu mkubwa,” Salasya aliandika.
Aidha, mwanasiasa huyo kutoka chama cha DAP-K alisema kwamba
atakuwa anatumia ufuasi huo mkubwa kama jukwaa la kutoa elimu ya kiraia kwa
wakenya ili kuwasaidia katika kufanya maamuzi bora kisiasa.
“Jukumu langu sasa litakuwa
kuwaelimisha wakenya elimu ya uraia na kuwafanya wafanye maamuzi sahihi katika
uongozi na Utawala wa ardhi hii.”
Salasya ambaye wiki mbili zilizopita alinaswa akitiririsha
moja kwa moja vikao vya bunge kwenye TikTok yake alitamba akisema kwamba
anahisi hivi karibuni atakuwa kama chombo cha habari kutokana na ufuasi mkubwa
anaozidi kupata kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
“Hivi karibuni nitakuwa
media house kwa sababu ya ufuasi mkubwa wa wakenya. Endelea kufuatilia endelea
kutoa maoni yako endelea kushare kile unachoona ni kizuri kwako,” Salasya alisema.