
MBUNGE wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amesema anafikiri ucheshi, upekee, akili, na hekima nyingi aliyo nayo zitakuwa sababu kuu za kumfanya kuenda mbinguni baada ya kutumikia taifa kama rais siku za usoni.
Mbunge huyo wa chama cha DAP-K alisema haya wikendi iliyopita
wakati akizungumza na wapiga kura wake katika eneo bunge lake kaunti ya
Kakamega.
Salasya alisema kwamba vigezo hivyo vitamfanya kuwa miongoni
mwa wachache ambao watakwenda mbinguni huku akijipigia debe kuwa rais mzuri
zaidi ambaye atalihudumia taifa tangu Kenya kuzaliwa mwaka 1963.
“Nadhani mimi ni mcheshi
wa kipekee mwenye akili na hekima ya Mungu. Nitaenda mbinguni baada ya
kutumikia nchi yangu ya Kenya kwa bidii. Nitakuwa rais bora wa kenya nimepata
tangu uhuru,” Salasya alisema.
Mbunge huyo bila kutaja atakuwa rais wa awamu ya ngapi,
alisisitiza kwamba atakuwa rais mchapakazi kumshinda marehemu Mwai Kibaki –
rais wa 3 anayetajwa kuwa rais aliyeleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo
nchini kati ya 2007 na 2013.
“Nitamshida hata Kibaki
kwa sababu ya moyo wangu mzuri wa kumtumikia kila mtu na kuona nchi yangu taifa
langu likiwa na nguvu na bora nitakuwa rais wa kihistoria ambaye sitasahaulika kwa
miaka 1,000 ijayo,” aliongeza.
Mbunge huyo ambaye yuko bungeni kwa muhula wake wa kwanza
amekuwa akidokeza kuhusu nia yake ya kuliwakilisha taifa la Kenya katika
wadhifa wa juu zaidi nchini katika siku za mbeleni.
Salasya amekuwa ni mwiba katika uongozi wa serikali ya Ruto,
ambapo kutoka ukanda wa Magharibi mwa Kenya ni miongoni mwa wachache
wanaosimama na kupinga sera za Kenya Kwanza wazi wazi.
Mwezi jana wakati wa ziara ya siku 5 ya kimaendeleo ya rais
Ruto katika ukanda huo, Salasya alimwambia bayana kuhusu changamoto za bima ya
mataifa, SHA akisema kwamba rais haambiwi ukweli.
Salasya alimtaka Ruto kumpa nafasi ya kuwa mshauri wake
kuhusu mambo ya kweli kwenye ‘ground’ haswa kuhusu SHA.