Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya ameagizwa kuhakikisha kuwa maafisa waliovalia kiraia hawafuniki nyuso zao wanapokabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano.
Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alisema Inspekta Jenerali anapaswa kuhakikisha zaidi kuwa maafisa wake hawafichi kitambulisho au usajili wa gari lolote linalotumiwa wakati wa kushughulika na watu wanaoandamana.
Jaji alitoa maagizo hayo kufuatia ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini Kenya LSK.
LSK kupitia kwa wakili Dudley Ochiel iliambia mahakama kutumwa kwa maafisa waliovalia mavazi ya kiraia kila mara kunaleta hali ya sintofahamu ambayo hatimaye inazuia haki ya watu kuandamana.
"Maafisa hawa ambao hawajatambuliwa hawawezi kuwajibika kwa matendo yao. Matokeo yake wanaishia kutumia nguvu kupita kiasi. Hawawezi kuwajibika kwa sababu hawajulikani," alisema Ochiel.
Alimwambia Jaji kwamba isipokuwa mahakama kuingilia kati na mwelekeo huo kukomeshwa, Wakenya wana hatari ya kifo na kunyimwa haki zao kwa mujibu wa katiba.
Jaji Bahati ambaye aliidhinisha suala la LSK kuwa la dharura aliagiza IG kuhakikisha kuwa kuna utiifu kamili katika suala la kuhakikisha kwamba maafisa wote waliovalia sare wataweka majina yao katika sare walizovalia kila wakati au nambari ya huduma inayotambulika.