MWANAUME mmoja raia wa Nigeria ambaye amekaa kwa muda
wa miaka 10 kwenye hukumu ya kifo kwa kuiba kuku na mayai ameahidiwa kusamehewa
na gavana wa jimbo la Osun kusini-magharibi.
Segun Olowookere alikuwa na umri wa miaka 17 mwaka wa
2010 alipokamatwa pamoja na mwandani wake, Morakinyo Sunday.
Inasemekana walishambulia nyumba ya afisa wa polisi
na mtu mwingine wakiwa na bunduki ya kizamani ya mbao na upanga lakini
wakatoroka tu na kuku.
Mnamo 2014, Jaji Jide Falola wa Mahakama Kuu ya Jimbo
la Osun aliwahukumu wawili hao kifo kwa kunyongwa baada ya kuwapata na hatia ya
kuvunja kwa nguvu nyumba ya afisa huyo wa polisi na kuiba mali yake.
Kulikuwa na kilio kote Nigeria wakati huo kwani wengi
walihisi hukumu hiyo ilikuwa kali sana.
Wawili hao baadaye walihamishwa hadi katika gereza
maarufu la ulinzi mkali la Kirikiri katika jimbo la Lagos ambako wamekuwa
katika mrengo wa kunyongwa.
Katika taarifa Jumanne, gavana Ademola Adeleke
aliagiza Olowookere asamehewe kwani ni muhimu kulinda utakatifu wa maisha.
“Nimemuagiza
Kamishna wa Haki aanzishe michakato ya kutoa haki ya huruma kwa kijana huyo.”
"Osun
ni nchi ya haki na usawa. Lazima tuhakikishe usawa na ulinzi wa utakatifu wa
maisha," gavana alichapisha kwenye X.
Hatima ya Morakinyo Sunday, ambaye alihukumiwa
kifungo pamoja na Olowookere, haijulikani kwa vile jina lake halikutajwa kwenye
taarifa hiyo.
Kwa miaka mingi, wazazi wa Olowookere, mashirika ya
kutetea haki za binadamu na Wanigeria wengine wamepigania kuachiliwa kwake.
Wazazi wake hivi majuzi walikuwa kwenye podikasti
ambapo walilia na kuomba mtoto wao wa pekee asamehewe.
Anatarajiwa kuachiliwa mapema mwaka wa 2025.
Nigeria haijatekeleza hukumu ya kifo tangu mwaka 2012
lakini kwa sasa kuna zaidi ya watu 3,400 wanaosubiri kunyongwa.