
Mahakama kuu imepuuzilia mbali uamuzi wa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula kuwa muungano wa Kenya Kwanza ndio upande wa wengi katika Bunge hilo.
Jopo la majaji watatu lililojumuisha Majaji John Chigiti, Jairus Ngaah na Lawrence Mugambi liliamua kuwa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ndio muungano wa wengi katika Bunge la Kitaifa.
Katika uamuzi wa kihistoria, mahakama ilisema Wetangula alikosea alipoupa muungano wa Kenya Kwanza wanachama 14 wa muungano wa Azimio ambao walikuwa wamejiuzulu kutoka kwa huo.
Wetangula alidai kuwa wanachama kadhaa wa Azimio waliiandikia afisi yake kusitisha uhusiano wao na chama cha Azimio la Umoja One Kenya.
Wabunge hao 14 walitoka katika vyama 4 chini ya Azimio, ambavyo ni United Democratic Movement (UDM), Movement for Democracy and Growth (MDG), Maendeleo Chap Chap (MCC) na Pamoja African Alliance (PAA).
Lakini jopo la majaji hao lilisema alipotia saini hati ya kiapo mahakamani kupinga kesi hiyo, hakutoa ushahidi wowote wa makubaliano yoyote ya baada ya uchaguzi yanayohusisha vyama vilivyotajwa na muungano wa KK.
Wetangula alidai kuwa vyama hivyo vilitia saini na kuweka kwa msajili wa vyama vya siasa mikataba hiyo.
Lakini majaji walikariri kwamba kwa kukosekana kwa uthibitisho wowote, uamuzi wa Wetang'ula hauwezi kuruhusiwa kusimama.