MWANAHABARI mmoja nchini Zimbabwe amezuiliwa na vyombo vya dola baada ya kufanya mahojiano na mkosoaji mmoja wa rais wa taifa hilo ambaye alimtaka kujiuzulu kwa kushindwa kuwafanyia wananchi kazi.
Kwa mujibu wa majarida kutoka Harare, Blessed Mhlanga,
mwanahabari maarufu wa kituo cha Televisheni cha mitandaoni, Heart and Soul
(HStv), amekuwa kizuizini tangu Februari 24 alipokamtwa.
Polisi walianzisha msako wa nchi nzima kumtafuta Mhlanga
kufuatia mahojiano yake na Blessed Geza, kigogo wa chama tawala cha Zanu-PF na
pia mkosoaji wa chama hicho, Januari 27 na Februari 11.
Geza, mkongwe wa vita vya ukombozi wa nchi hiyo
vilivyopelekea uhuru mwaka 1980, alisema katika mahojiano hayo kwamba rais
Emmeson Mnangagwa anapaswa kujiuzulu.
Pia alilaani mrengo wa Zanu-PF ambao umeripotiwa kupigia debe
mipango ya kubadilisha katiba ili kumruhusu Mnangagwa, 82, kugombea muhula wa
tatu.
Baada ya mahojiano hayo yenye ukakasi mwingi, kigogo huyo wa
vita vya ukombozi wa Zimbabwe alichimba mitini na polisi walisema bado
wanamsaka kwa udi na uvumba.
Waendesha mashtaka walisema mwanahabari huyo alichochea
vurugu kupitia mahojiano yake na kuiomba mahakama kumzuilia kwa saa 72 ili
kuruhusu uchunguzi zaidi.
"Ikiwa mshtakiwa atapewa dhamana, ataingilia
mashahidi," mwendesha mashtaka alisema.
Amnesty International ililaani kukamatwa kwa Mhlanga na
kutaka kuachiliwa kwake mara moja na kufutwa kwa mashtaka yote bila masharti.
"Uandishi wa habari
sio uhalifu, na watendaji wa vyombo vya habari wanapaswa kufanya kazi zao bila
hofu ya kulipizwa kisasi," shirika la kimataifa la haki za
binadamu lilisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii.
Jukwaa la Kitaifa la Wahariri wa Zimbabwe lilisema
"limefadhaishwa na kuhuzunishwa sana" na kukamatwa kwake, ambayo ni
sawa na unyanyasaji wa mwandishi wa habari anayefanya kazi yake "kwa
maslahi ya umma".
Zimbabwe imeorodheshwa katika nafasi ya 116 kati ya nchi 180
katika Maripota Wasio na Mipaka (RSF) 2024 World Press Freedom Index.
Vyombo vya habari "vimekabiliwa na mateso zaidi"
tangu Mnangagwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2023, kulingana na
RSF yenye makao yake Paris.