
Katika kile kinachoonekana kama safari ya matumaini yasiyoisha, Prince Al-Waleed bin Khaled bin Talal – maarufu kama "Mwana wa Kifalme aliyelala" – alitimiza miaka 36 mnamo Aprili 18, 2025, akiwa bado katika hali ya kupoteza fahamu tangu apate ajali mbaya ya gari miaka ishirini iliyopita.
Ajali hiyo ilitokea mwaka 2005 wakati Al-Waleed alikuwa mwanafunzi katika chuo cha kijeshi jijini London, ambapo alijeruhiwa vibaya kichwani na kupata damu kuvuja katika ubongo.
Tangu siku hiyo, amekuwa akihifadhiwa kwenye mashine za kusaidia uhai katika Hospitali ya King Abdulaziz Medical City jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Licha ya ushauri wa madaktari wa kuacha huduma za uhai, baba yake, Prince Khaled bin Talal, amekataa katakata, akiendelea kuamini kwamba mwanawe anaweza kupona.
"Kama Mwenyezi Mungu alitaka afe kwenye ajali, angekuwa kaburini sasa," amesema kwa imani kuu na moyo wa kifamilia wa kupigiwa mfano.
Kwa kipindi chote hiki, Prince Al-Waleed anaripotiwa kuonyesha ishara ndogo za uhai kama kuinua kidole au kugeuza kichwa, lakini bado hajarejea fahamu kikamilifu. Baba yake ameendelea kuwa karibu naye kila siku, kimya kimya akiwa na matumaini thabiti.
Siku yake ya kuzaliwa mwaka huu ilichochea hisia kali kwenye mitandao ya kijamii, ambapo watu kutoka pembe mbalimbali za dunia walituma jumbe za maombi na picha za kumbukumbu akiwa na familia.
Shangazi yake, Princess Rima bint Talal, alishiriki ujumbe wa kugusa moyo kwenye mtandao wa X (zamani Twitter): “Mpendwa wangu Al-Waleed, miaka ishirini na moja lakini bado umo moyoni mwetu. Ee Mwenyezi Mungu, mponye mja wako Al-Waleed.”
Prince Al-Waleed ni mjukuu wa Prince Talal bin Abdulaziz na kitukuu cha Mfalme Abdulaziz, mwanzilishi wa taifa la Saudi Arabia. Ingawa hana nafasi ya moja kwa moja kwenye uongozi wa sasa, uhusiano wake wa kifamilia unamfanya kuwa jamaa wa karibu wa Mfalme wa sasa, Salman bin Abdulaziz.
Hali yake imekuwa mfano wa uvumilivu kwa familia yake na watu wengi wanaoendelea kusali na kutumaini miujiza ya kitabibu katika siku za usoni. Hadi sasa, bado anatumia mashine ya kumsaidia kupumua pamoja na bomba la kumlisha.
Prince Al-Waleed anasalia kuwa
ishara ya upendo wa familia usioyumba na tumaini lisilokoma.