Amos Kimunya afichua maelezo kuhusu marehemu mkewe, tarehe ya mazishi

Bi Lucy Wanjiru Muhinga atazikwa siku ya Ijumaa Februari 2, 2024, familia imetangaza.

Muhtasari

•Familia ilitangaza kwamba mkutano utafanyika Alhamisi jioni kabla ya mazishi kufanyika Ijumaa katika madhabahu ya Consolata.

•Maelezo ya historia ya familia ya marehemu yalishirikiwa katika taarifa hiyo ikiangazia watu wanaohusiana naye na wale anaowaacha.

na marehemu mkewe
Amos Kimunya na marehemu mkewe
Image: HISANI

Mke wa mwanasiasa Amos Kimunya, Bi Lucy Wanjiru Muhinga atazikwa siku ya Ijumaa Februari 2, 2024, familia imetangaza.

Katika taarifa ya Jumatano, familia ya Kimunya ilitangaza kwamba mkutano wa familia na marafiki utafanyika kwanza siku ya Alhamisi jioni kabla ya mazishi kufanyika katika madhabahu ya Consolata.

“Familia na marafiki watakutana Alhamisi tarehe 1 Februari 2024 saa kumi na moja jioni katika Ukumbi wa Consolata Shrine Westlands kwa mkutano wa Maombi. Misa ya mazishi itafanyika Ijumaa tarehe 2 Februari 2024 katika Madhabahu ya Consolata,” familia ilisema katika taarifa.

Familia ya Kimunya iliomboleza marehemu Lucy kama mke mpendwa, mama na nyanya.

Maelezo ya historia ya familia ya marehemu yalishirikiwa katika taarifa hiyo ikiangazia watu wanaohusiana naye na wale anaowaacha.

“Marehemu ni mke wa Mhe Amos Muhinga Kimunya, bintiye marehemu Iringu Kahonge na Gladys Munjiru. Mkaza mwana wa marehemu Samuel Kimunya na Maria Muthoni Kimunya. Mama kwa Tabitha Muhinga Kibaara & Ronald Kibaara Meru. Nyanya kwa Kendi, Gitonga, Macharia, marehemu Faith Muthoni, marehemu Eliud Ndegwa na Evelyn Njoki,” familia hiyo ilisema.

Pia walitaja kwamba alikuwa shemeji wa watu wengi.

Bw Amos Kimunya alitangaza kifo cha mkewe siku ya Jumanne.

Katika taarifa yake, kiongozi huyo wa zamani wa wengi bungeni alitangaza kuwa mkewe alifariki usiku wa kuamkia Jumanne.

Mbunge huyo wa zamani wa Kipipiri alifichua kuwa marehemu Lucy alikuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi alipokata roho.

"Ni kwa huzuni kubwa na kukubali kwa unyenyekevu mapenzi ya Mungu kwamba ningependa kutangaza kwamba Jumanne hii asubuhi saa tisa asubuhi mke wangu mpendwa Lucy alienda kuwa na bwana, alipokuwa akipokea huduma katika Hospitali ya Nairobi," Amos Kimunya alitangaza kupitia mtandao wa Facebook.

Mwanasiasa huyo aliendelea kuzungumzia nafasi kubwa ambayo marehemu alicheza katika maisha yake na jamii kwa ujumla.

"Alikuwa nguzo muhimu katika maisha yangu ya kibinafsi na ya kisiasa, alichangia pakubwa kuifanya jamii yetu kuwa ya kijani kibichi kupitia mipango mbalimbali na kuunga mkono vijana na wanawake," alisema.

Aliongeza, “Nenda sawa mpendwa wetu Lucy, tutakukumbuka sana. Mawasiliano zaidi yatafuata."

Makumi ya Wakenya walimiminika kumfariji Bw Kimunya na familia yake huku wakimuomboleza mpendwa wao.