Ngong: Mzee wa miaka 76 azirai na kufariki baada ya polisi wa trafiki kumsimamisha

Mzee alikuwa anaendesha kabla ya polisi 5 wa trafiki kumsimamisha, mmoja akaingia ndani na baada ya muda mfupi akatoka kwa haraka akionekana kuwa na wasiwasi na kuita gari la polisi kumkimbiza hospitalini.

Muhtasari

• Dereva mmoja wa lori aliambia jarida hilo kwamba mzee huyo alitoka ndani ya gari lake akiwa na noti ya elfu moja huku akitafuta mwenye angemsaidia kuivunja.

Mchoro wa afisa wa trafiki
Mchoro wa afisa wa trafiki
Image: The Star (Mchoro)

Dereva mmoja mzee mwenye umri wa kati ya miaka 70-79 ameripotiwa kuanguka sakafuni, kuzirai na kufariki baadae baada ya kusimamishwa na afisa wa trafiki katika barabara ya Ngong kuelekea Kiseriani Ijumaa asubuhi.

Kulingana na taarifa za awali, mzee huyo alikuwa anaendesha gari lake baada ya afisa wa trafiki kumsimamisha katika kile kilitajwa kuwa polisi huyo alikuwa anaitisha hongo.

Kwa mujibu wa jarida la Nation, polisi wa trafiki walikuwa watano na wawili wao walilikagua gari hilo kwa haraka kabla ya kuitisha kile kilichodhaniwa kuwa ni hongo kutoka kwa mzee huyo.

Afisa mmoja aliingia ndani ya gari hilo na kumtaka mzee huyo kuendesha kwa umbali wa mita 100 ambapo ilidhaniwa kuwa ni duka la M-Pesa walikuwa wanatafuta ili atoe pesa na kumpa.

Dereva mmoja wa lori aliambia jarida hilo kwamba mzee huyo alitoka ndani ya gari lake akiwa na noti ya elfu moja huku akitafuta mwenye angemsaidia kuivunja kwani alikuwa ameelewana na polisi huyo kwamba angempa shilingi 200 kama mlungula.

Kipindi hicho chote polisi alikuwa ndani ya gari lake akiwa amesubiria chai yake na mzee alipopata kuivunja ile 1000, alirudi kwa gari lake lakini ni kama hawakuelewana na polisi yule alionekana akishuka kwa haraka kabla ya kuita gari la polisi na kumkimbiza mzee yule hospitalini.

Kwa bahati mbaya mzee huyo alifariki dunia wakati anakimbizwa hospitalini, kulingana na jarida hilo.

Hata hivyo, kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Ngong alisema kuwa mzee huyo alifariki na familia yake ilisema amekuwa na matatizo ya kupumua tangu ujio wa Covid-19, akiwatetea polisi wake dhidi ya madai ya kuitisha hongo iliyosababisha mshtuko wa mzee.