Aliyekuwa mtangazaji Salim Swaleh aomba msamaha baada ya kukumbwa na kesi ya ulaghai

Mwanahabari huyo alisema miezi iliyopita imekuwa ngumu kwake na ameshindwa hata kutoka nje ya nyumba yake.

Muhtasari

•Swaleh alituma ujumbe kwa njia ya video akisema alivunja uaminifu mkubwa ambao ulijengwa kwa miaka mingi na anasikitika.

•Swaleh na wenzake wanne wanadaiwa kula njama ya kulaghai Sh5.8 milioni kutoka kwa kampuni ya ushauri.

Bw Salim Swaleh, aliyekuwa mkurugenzi wa vyombo vya habari katika afisi ya Waziri Mkuu na Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.
Image: HISANI

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma ya Vyombo vya Habari katika ofisi ya Mkuu wa Mawaziri Salim Swaleh sasa anaomba msamaha.

Mtangazaji huyo wa zamani wa habari alituma ujumbe kwa njia ya video akisema alivunja uaminifu mkubwa ambao ulijengwa kwa miaka mingi na anasikitika.

"Mheshimiwa, umekuwa kama baba yangu kwa muda mrefu zaidi ambao nimekujua. Tumejenga uaminifu usio na kifani kati yetu na kwa muda wa mwaka mmoja na nusu uliopita nimekutumikia, nimetumikia ofisi yako nzuri, na kukutumikia kwa bidii isiyo na kifani. Nilivunja uaminifu na ninasikitika sana kuhusu hilo. Hakika nimejuta kuhusu hilo,” Swaleh alisema kwa hisia nyingi kwenye video hiyo.

Mwanahabari huyo alisema miezi iliyopita imekuwa ngumu kwake na ameshindwa hata kutoka nje ya nyumba yake.

Alisema hii ni kwa sababu ya umaarufu mbaya alizopata na hata amefikiria kujitoa uhai.

"Mwezi uliopita umekuwa mgumu sana kwangu. Nimeshindwa hata kutoka kwa sababu ya aina ya umaarufu niliopokea, kila kitu ambacho watu walisema kunihusu kilinitupa tu katika eneo ambalo halijajulikana. Mambo mengi yamekuwa yakienda akilini mwangu, mambo mabaya sana, wakati mwingine ninahisi kujitoa uhai,” alisema.

Swaleh aliongeza kuwa alipoteza kila kitu kwa haraka na kwamba bili pia zimekuwa changamoto kubwa kwake kwani zinaongezeka.

Mwanahabari huyo alisema kuwa mshahara wake ulisimamishwa na ana mikopo inayohitaji kulipwa.

"Ni mwisho wa mwezi, bili zinarundikana, mishahara imesimamishwa ghafla, nina mikopo, tafadhali itafute katika moyo wako unisamehe," alisema.

Aliongeza, “Pili, naomba unisaidie kumaliza hili ili nichukue vipande vidogo vilivyobaki nione nianzie wapi. Kwa aina ya umaarufu mbaya niliopata, karibu haiwezekani kupata mahali pengine pa kufanya kazi. Tafadhali nihurumie.”

Kulingana na hati ya mashtaka, Swaleh na wenzake wanne wanadaiwa kula njama ya kulaghai Sh5.8 milioni kutoka kwa kampuni ya ushauri.

Kosa hilo linasemekana kutendeka kwa tarehe tofauti kati ya Juni 4, 2014, na Juni 22, 2014, katika ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, haswa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Vyombo vya Habari, ndani ya kaunti ya Nairobi.