KESI YA BBI

Jaji Musinga aomba wahusika kwenye kesi ya BBI kuzingatia heshima

Rais wa mahakama ya kukata rufaa nchini Kenya,Daniel Musinga amesema kuwa jopo la majaji saba litateuliwa kuskiza kesi dhidi ya maamuzi ya BBI.

Muhtasari

•Wakili Ochiel alitaka majaji watatu wa mahakama ya kukata rufaa kufanya maamuzi kuhusiana na matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya idara ya mahakama.

Rais alisema kuwa mahakama ilikuwa imepindua matakwa ya Wakenya na kuwanyima haki yao ya kupiga kura kwenye kura ya maoni. 

RAIS WA MAHAKAMA YA KUKATA RUFAA DANIEL MUSINGA
RAIS WA MAHAKAMA YA KUKATA RUFAA DANIEL MUSINGA
Image: MAKTABA

Rais wa mahakama ya kukata rufaa nchini Kenya,Daniel Musinga ameagiza wahusika wote kwenye kesi ya BBI kuzingatia heshima na kuruhusu mahakama kufanya kazi yake.

Hii imetokana suala lililotajwa mbele ya mahakama hiyo na wakili Ochiel kuhusiana na matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya idara ya mahakama.

Rais Kenyatta alisema kuwa idara ya mahakama ilikuwa imejaribu mipaka ya katiba ya Kenya kutoka kutupiliwa mbali kwa matokeo ya Urais mwakani 2017 hadi kutupiliwa mbali kwa mchakato wa BBI. Rais alisema kuwa mahakama ilikuwa imepindua matakwa ya Wakenya na kuwanyima haki yao ya kupiga kura kwenye kura ya maoni.

Wakili Ochiel alitaka majaji tatu wa mahakama ya kukata rufaa, Roseline Nambuye, Daniel Musinga na Hannah Okwengu kufanya maamuzi kuhusiana na matamshi hayo. Ochiel alitaka matamshi hayo kuondolewa.

Naomba tuheshimiane sote na tusianze  kuhukumu kesi hii kwenye vyombo vya habari. Wacha turuhusu mahakama kufanya maamuzi ya kisawa bila mashambulizi na maoni yoyote kutoka kwa wahusika kwenye kesi hii” Musinga alisema.

Musinga pia ametangaza kuwa jopo la majaji saba litateuliwa kuskiza kesi dhidi ya maamuzi ya BBI. 

Musinga ametaka wahusika wote kuleta mawasilisho ya kati ya kurasa 20-25.