Mwanamke asakwa na DCI kuhusiana na mauaji ya mkurugenzi wa fedha wa Nairobi hospital

Kulingana na DCI, wachunguzi pia walipata vitu vya mauaji katika eneo la tukio. Vitu hivyo vimefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.

Muhtasari
  • Katika taarifa iliyochapishwa Alhamisi, Septemba 21, DCI pia ilisambaza picha za skrini za mwanamke anayeaminika kuwa mshukiwa wa mauaji.
Mwanamke asakwa na DCI kuhusiana na mauaji ya mkurugenzi wa  fedha wa Nairobi hospital
Image: DCI/X

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inaomba usaidizi wa kumkamata mwanamke anayedaiwa kumuua Mkurugenzi wa Fedha anayefanya kazi katika Nairobi hospital.

Katika taarifa iliyochapishwa Alhamisi, Septemba 21, DCI pia ilisambaza picha za skrini za mwanamke anayeaminika kuwa mshukiwa wa mauaji.

Picha zilizoshirikiwa na DCI zilionyesha mwanamke huyo akiruka kutoka kwa uzio wa nyumba ya Daktari baada ya kutekeleza uhalifu huo katika eneo la Woodley Estate, Nairobi.

"Kufuatia mauaji ya kutisha ya Dkt. Erick Maigo, mnamo Ijumaa Septemba 15, 2023, maafisa wa upelelezi wanaomba habari zinazoweza kusababisha kukamatwa kwa mwanamke ambaye picha zake zinaonekana hapa chini.

"Mshukiwa ambaye alinaswa akiondoka katika makazi ya mwathiriwa huko Woodley Annex -Upper anaaminika kuhusika katika mauaji hayo ambayo yalikuwa machafu zaidi kabla ya kutoroka kupitia mlango wa nyuma," taarifa ya DCI ilisoma kwa sehemu.

Kulingana na DCI, wachunguzi pia walipata vitu vya mauaji katika eneo la tukio. Vitu hivyo vimefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.

Wachunguzi pia walikusanya sampuli ya damu kutoka kwa nyumba hiyo. Walifichua kuwa sampuli hizo zitatumika kumweka mshukiwa katika eneo la uhalifu.

"Visu viwili vilivyokuwa na damu vinavyoaminika kuwa silaha za mauaji vilipatikana katika eneo la uhalifu.

"Huku wapelelezi wakichoma mafuta ya usiku wa manane ili kumkamata mshukiwa wa kike, wananchi wanaombwa kujitolea kutoa taarifa zozote ambazo zinaweza kumfanya akamatwe mara moja," DCI iliomba.

Mwili wa Daktari huyo ambaye pia alifanya kazi kama Mkurugenzi wa Fedha, ulipatikana Ijumaa, Septemba 15, ukiwa na majeraha mengi ya kuchomwa visu.