Saudi Arabia yaahirisha kunyongwa kwa raia wa Kenya

Stephen Munyakho, mwana wa mwanahabari mkongwe Dorothy Kweyu, alihukumiwa kifo mwaka wa 2011.

Muhtasari

• Mkenya anayetarajiwa kunyongwa nchini Saudi Arabia amepata ahueni ya dakika za mwisho kufuatia kampeni kubwa ya mitandao ya kijamii.

• Siku ya Jumatatu, siku mbili tu kabla ya Munyakho kunyongwa, Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa Kenya alisema Saudi Arabia "imekubali" ombi la serikali la kuahirisha kifo.

Image: Bring Back Stevo campaign

Mkenya anayetarajiwa kunyongwa nchini Saudi Arabia amepata ahueni ya dakika za mwisho kufuatia kampeni kubwa ya mitandao ya kijamii.

Stephen Munyakho, mwana wa mwanahabari mkongwe Dorothy Kweyu, alihukumiwa kifo mwaka wa 2011 kufuatia mapigano makali na mwenzake katika taifa la Ghuba.

Kulingana na kampeni ya Bring Back Stevo, inayoendeshwa na wafuasi wa Munyakho, wafanyakazi wote "walipata majeraha ya kuchomwa kisu" lakini ni Munyakho, pekee ndiye aliyenusurika.

Kwa hiyo, Munyakho, alihukumiwa kifo.

Chini ya sheria za Saudia, hukumu ya kifo inaweza kuondolewa ikiwa familia itakubali kulipwa fidia badala yake.

Familia yake ya nyumbani nchini Kenya imekuwa ikijaribu kutafuta pesa zinazohitajika, ambazo ni riyal milioni tatu na nusu za Saudia (dola 940,000), kwa ajili ya familia ya marehemu, ili kumuokoa Munyakho.

Siku ya Jumatatu, siku mbili tu kabla ya Munyakho kunyongwa, Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa Kenya alisema Saudi Arabia "imekubali" ombi la serikali la kuahirisha kifo hicho ili kuruhusu "mazungumzo zaidi kati ya pande zote".

Korir Sing'Oei aliandika kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii X: "Tunapopanga mikakati ya kuleta jambo hili kwa hitimisho linalokubalika zaidi, na hivyo kuzipa familia zote mbili mwisho wanaohitaji na kustahili, tutaendelea kuegemea kwa thabiti urafiki tulio nao na washirika wetu wa Saudia, na pia kwa nia njema ya Wakenya wote."