Azma ya Raila Kuwa mwenyekiti wa AUC yapigwa jeki

Raila anatafuta kumrithi Moussa Faki Mahamat kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Muhtasari

• Raila atachuana na Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, Anil Kumarsingh Gayan wa Mauritius na Richard Randriamandrato wa Madagascar.

Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na Rais wa DRC Felix Tshisekedi.
Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na Rais wa DRC Felix Tshisekedi.
Image: RAILA ODINGA/X

Azma ya kinara wa upinzani Raila Odinga kuwania uwenyekiti wa  Tume ya Umoja wa Africa (AUC) imepigwa jeki tena baada ya taifa la DRC kuahidi kumuunga mkono.

Kupitia ukurasa wake wa X, Raila alisema alikutana na rais Felix Tshisekedi wa DRC na baada mashauriano Tshisekedi alitangaza kumuunga mkono Raila katika azma yake ya kuwania wadhifa wa menyekiti wa AUC.

“Nilikutana na Rais wa DRC Felix Tshisekedi leo kujadili azma yangu ya AUC. Mazungumzo yetu yalijikita katika masuala ya msingi ya usalama, maendeleo, na mabadiliko ya hali ya hewa—muhimu kwa ajili ya kuleta ustawi wa kudumu na kuendeleza mustakabali wetu wa pamoja. Ninamshukuru kwa uthibitisho wake,” Raila aliandika kwenye ukurasa wake wa X.

Wakati wa mkutano huo rais Tshisekedi pia aliahidi kwamba serikali yake itampigia debe Raila ili kuhakikisha anatwaa ushindi.

Tangu atangaze azma yake kuwania uwenyekiti wa AUC Raila tayari amepokea uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbali mbali wa kandaa hii na nje.

Raila atachuana na Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, Anil Kumarsingh Gayan wa Mauritius na Richard Randriamandrato wa Madagascar.

Raila anatafuta kumrithi Moussa Faki Mahamat kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Amekuwa akipokea wajumbe kutoka duniani kote katika ofisi yake, huku akipigia debe kuungwa mkono kwa kiti hicho.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Fawzia Yusuf Adam pia ametangaza kumuunga mkono Raila kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Fawzia ambaye alikuwa akiwania kiti hicho alitangaza kumuunga mkono Raila baada ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Uchaguzi wa Mwenyekiti ajaye wa AUC utafanyika Januari 2025, ukiwiana na mwisho wa muhula wa Faki.