Kaimu waziri wa jinsia Musalia Mudavadi
amemteua Kapteni Mstaafu Kungui Muigai kwenye kazi ya serikali.
Mudavadi katika notisi ya gazeti la
serikali ya Januari 24, alimteua Muigai kama mwanachama wa Baraza la Kituo cha
Utamaduni cha Kenya.
Muigai, ambaye ni binamu wa rais wa zamani Uhuru Kenyatta, atahudumu katika wadhifa huo kwa muda wa miaka mitatu.
Kazi yake itaanza mara moja.
"Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Kituo cha Utamaduni cha Kenya, waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi, anateua tena- Kungu Muigai kuwa mwanachama wa Baraza la Kituo cha Utamaduni cha Kenya, kwa muda wa miaka mitatu (3), kuanzia tarehe 24 Januari, 24, 2025," notisi ya Gazeti ilisema.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba naye alimteua Francis Meja kama mwanachama wa Baraza la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Murang’a, kuanzia Januari 20, 2025.
Muigai mnamo Februari mwaka jana alitoa
wito kwa wakazi wa Mlima Kenya kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza.
Kung'u alisema kuwa serikali inafaa kupewa muda wa kutosha kutekeleza ahadi zake za kampeni.
"Tunafaa kuunga mkono serikali badala ya kuikosoa kila siku na huu ni wito wa wazi kwa watu na viongozi wote wa Mlima Kenya," alisema.
"Serikali ilichukua madaraka, na ni wakati sasa kila mtu afanye kazi yake na wengine wasubiri uchaguzi 2027. Huyo mtu anayekwambia serikali inaweza kuanguka, serikali hazianguki hata ikiongozwa na mtu kijana usicheze nayo," aaliongeza.
Kung'u Muigai pia anatambuliwa kama msimamizi wa Baraza la Wazee wa Kikuyu.