
Rais William Ruto mnamo Jumapili
alikaribisha sera rasmi ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutambua tu jinsia
ya kiume na ya kike.
Rais alisema anafurahi kwamba demokrasia kuu zaidi duniani imechukua hatua haraka kutoa ufafanuzi juu ya suala ambalo limezua utata hapo awali.
“Kinyume na siku za nyuma, Marekani imekaribisha maendeleo fulani ambayo yanasisitiza mwelekeo wa kisera ulio wazi; wavulana wabaki kuwa wavulana, wanaume wabaki wanaume, wasichana wabaki wasichana, na wanawake wabaki wanawake,’’ Ruto alisema.
Akiongea wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa kuu la The Global Cathedral jijini Nairobi, Ruto alisisitiza haja ya kukumbatia sera ya wanawake na wanaume pekee.
"Tumepata kuelewa kwamba mwelekeo wa sera za Marekani unaunga mkono kile tunachoamini," Rais Ruto alisema.
“Tunamshukuru Mungu kwamba mwaka huu,
habari za kwanza kabisa kutoka Marekani katika utawala mpya ni kuthibitisha
yale ambayo Biblia inasema, imani yetu inaamini nini na mapokeo yetu
yanategemea msingi gani.’’
Wiki iliyopita Rais Trump alitia saini amri za utendaji zinazothibitisha kwamba Marekani itatambua jinsia mbili pekee, wanaume na wanawake, ambazo hazibadiliki.
"Tutaunda jamii isiyozingatia rangi na inayozingatia sifa. Kuanzia leo, itakuwa sera rasmi ya serikali ya Marekani kwamba kuna jinsia mbili pekee, wanaume na wanawake," Trump alisema katika hotuba yake ya kuapishwa.
Rais Trump aliamuru Jumatatu iliyopita alipokuwa akitaka kukomesha haraka sera mbalimbali zinazolenga kukuza usawa wa rangi na kulinda haki za watu wa LGBTQ+.
Agizo hilo linaitaka serikali kutumia neno "sex" badala ya "jinsia".
Pia inahitaji hati za utambulisho
zinazotolewa na serikali, ikiwa ni pamoja na pasipoti na visa, ziwe kulingana
na kile ilichoeleza kama "uainishaji wa kibayolojia usiobadilika wa mtu
kama mwanamume au mwanamke."