
Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, ametuma risala za rambirambi kwa Spika wa Seneti, Amason Kingi, kufuatia kifo cha baba yake mpendwa, Mzee Kingi Mwaruwa.
Kupitia ujumbe wake wa faraja, Rais Ruto amemtaja marehemu Mzee Mwaruwa kama mtu wa kuheshimika, mchapakazi, na mwenye maono makubwa.
Rais alisisitiza kwamba mchango wa marehemu kwa familia yake na jamii ya Kilifi utaendelea kukumbukwa kwa vizazi.
"Tunatoa pole zetu kwa Spika wa Seneti kufuatia kifo cha baba yake mpendwa, Mzee Kingi Mwaruwa. Alikuwa mtu anayeheshimika, mwenye maendeleo na mchapakazi. Mheshimiwa Amason Kingi, familia na watu wa Kilifi mpo katika maombi yetu wakati huu mgumu. Pumzika kwa amani," Ruto alisema.
Taarifa ya msiba wa Mzee Mwaruwa imeibua maombolezo na rambirambi kutoka kwa viongozi wa kitaifa, marafiki, na wananchi kwa ujumla.
Wengi wameeleza kuwa marehemu alikuwa kiongozi wa familia mwenye busara, ambaye alichangia pakubwa katika malezi na uongozi wa mwanawe, Spika Kingi.
Mbali na Rais Ruto, viongozi wengine wa kisiasa wameendelea kutuma risala za pole kwa familia ya Kingi, wakitambua mchango wa Mzee Mwaruwa katika jamii na msukumo wake kwa maendeleo ya watu wa Kilifi.
Katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, Rais Ruto amewataka familia ya Kingi na jamii kwa ujumla kushikamana na kumpa Spika Kingi faraja anapoomboleza kumpoteza baba yake.
Mzee Kingi Mwaruwa ataendelea kukumbukwa kwa mafunzo yake ya maisha, maadili, na mchango wake katika malezi ya familia yake.
Kwa mujibu wa Spika Kingi, marehemu alikuwa nguzo ya familia, mshauri wake mkuu, na mtu aliyempa msingi wa maono yake ya uongozi.
Katika taarifa yake ya kumuomboleza babake, Kingi alitoa pongezi kwa mafundisho na upendo alionao kutoka kwa baba yake, akisisitiza umuhimu wa kutokukata tamaa hata katika nyakati ngumu.
"Ulinifundisha mafunzo mengi ya thamani, na muhimu zaidi, ni kutokukata tamaa bila kujali. Ni somo hili lilikinisukuma hadi kufikia hapa. Hakika, ulikuwa zawadi ya Mungu kwetu. Sikuwa naweza kuomba baba bora Zaidi," Kingi aliandika kwenye X.
Taarifa yake ilimalizika kwa maneno ya faraja na matumaini kuhusu roho ya mzazi huyo wake, ambapo Kingi aliongeza,
"Baba, nawaombea malaika wafungue Milango ya Mbinguni na kumkaribisha malaika mwingine kwa dansi, kama tulivyofanya katika Mjanaheri. Mpaka tutakapokutana tena, Baba."
Kwa sasa, familia ya Kingi inaendelea kupanga taratibu za mazishi, huku taifa likiendelea kuwa pamoja nao katika maombi na mshikamano wa kiroho.