
Katika uamuzi uliotolewa katika Bunge la Kitaifa siku ya Jumatano, Spika Wetangula alieleza kuwa Mahakama haikutoa mwelekeo kuhusu ni upande upi ni wa wengi au walio wachache.
Alibainisha kuwa hali ilivyo bado haijabadilika kwani Kenya Kwanza inajumuisha wabunge 165 huku Azimio ikiwa na wabunge 154. Katika orodha hiyo Wetangula alipokonya Azimio wabunge katika vyama tanzu ambao walitangaza kuhama muungano huo.
Zaidi ya hayo, Wetangula aliagiza kukatwa kwa rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Uamuzi huo wa spika hata hivyo ulipingwa vikali na wabunge wa Azimio wakiongozwa na aliyeibua hoja hiyo Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.
"Kama Azimio kwa heshima kubwa hatukubaliani na mawasiliano yenu na kama Azimio tutachukua hatua zaidi," Odhiambo alisema.
Baada ya uamuzi huo kutolewa kwa gadhabu Wabunge wa Azimio walitoka nje ya Bunge.
Majaji John Chigiti, Lawrence Mugambi, na Jairus Ngaah wiki iliyopita walikosoa msimamo wa Spika Wetangula kwa kukinzana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa ambaye stakabadhi zake zilionyesha kuwa Azimio ilikuwa na wabunge wengi kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022 kabla ya wabunge 14 kugura na kujiunga na kujiunga na muungano tawala.