
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, mnamo siku ya Jumatano alihitimisha rasmi kampeni zake za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa ziara nchini Burundi.
Katika hatua yake ya mwisho kabla ya uchaguzi, Raila alikutana na viongozi wa serikali ya Burundi na wanadiplomasia kujadili ajenda yake kwa bara la Afrika.
Raila alipokewa na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, pamoja na viongozi wakuu wa serikali ya nchi hiyo jirani.
Mazungumzo yao yalijikita katika masuala ya ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiuchumi, na mageuzi ndani ya Umoja wa Afrika.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Raila alielezea matumaini yake ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Burundi na mataifa mengine ya Afrika.
“Tumekuwa na mazungumzo yenye manufaa kuhusu mustakabali wa bara letu. Afrika inahitaji uongozi thabiti na mwelekeo mpya ili kuimarisha mshikamano na maendeleo,” Raila alisema katika taarifa baada ya mkutano huo.
Katika kampeni zake, Raila amesisitiza ajenda ya kuimarisha uchumi wa Afrika kupitia biashara huru baina ya mataifa, kuboresha miundombinu, kuimarisha amani na usalama, pamoja na kufanya mageuzi katika Umoja wa Afrika ili kuongeza ufanisi wake.
Ameeleza kuwa bara la Afrika linahitaji mshikamano zaidi ili kukabiliana na changamoto kama migogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi, na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Tangu alipotangaza nia yake ya kugombea wadhifa huo, Raila ameendesha kampeni katika mataifa mbalimbali ya Afrika, akitafuta uungwaji mkono kutoka kwa wakuu wa nchi na wadau wa Umoja wa Afrika. Burundi ilikuwa moja ya vituo vya mwisho vya kampeni yake kabla ya uchaguzi kufanyika.
Uchaguzi wa Mwenyekiti wa AUC unatarajiwa kufanyika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika wikendi hii ijayo.
Raila anapambana na wagombea wengine kutoka mataifa tofauti ya Afrika, huku akiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa wakuu wa mataifa ya Afrika ambao watapiga kura kuamua ni nani atakayeongoza Tume ya Umoja wa Afrika kwa miaka ijayo.