logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Huzuni huku baba aliyedungwa kisu mbele ya mwanawe wa miaka 3 mtaani Mathare akizikwa Kisii

Marehemu ambaye alikumbana na kifo chake mnamo Januari 20 alipokuwa akimsindikiza mwanawe kwenda shuleni.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri14 February 2025 - 08:24

Muhtasari


  •  Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye alikuwepo kwenye mazishi hayo alisema kuwa tukio hilo lilijawa na huzuni nyingi.
  •  Sonko alisisitiza kuhusu uamuzi wake wa kumchukua mtoto huyo na kumtunza kama mtoto wake mwenyewe.

Mwanasiasa Mike Sonko akiwa na James wakati wa mazishi ya babake Kisii.
Michael Omworo Ombui, mwanamume aliyeuawa kwa kudungwa kisu na majambazi mbele ya mwanawe wa miaka mitatu katika eneo la Mathare Area 4, Nairobi hatimaye alizikwa Alhamisi, Februari 13.

Marehemu ambaye alikumbana na kifo chake mnamo Januari 20 alipokuwa akimsindikiza mwanawe kwenda shuleni alizikwa katika kijiji cha Kiamokama, eneo bunge la Nyaribari Masaba, kaunti ya Kisii.

 Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye alikuwepo kwenye mazishi hayo alisema kuwa tukio hilo lilijawa na huzuni nyingi.

 “Baby James ni mvulana mwenye nguvu sana. Tulimzika babake katika eneo bunge la Kiamokama, eneo bunge la Nyaribare Masaba katika hafla ya kuhuzunisha sana,” Sonko alisema kupitia X.

 “Niliwezesha na kulipia kikamilifu gharama za mazishi kutoka Nairobi. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Baby James kuzuru kijiji chake na hakuwa amekutana na babu na babu yake tangu kuzaliwa,” aliongeza.

 Katika taarifa yake, mwanasiasa huyo mwenye utata pia alizungumzia jinsi mtoto huyo wa miaka mitatu amebaki na kiwewe tangu kushuhudia babake akiuawa mwezi uliopita.

 Sonko alisisitiza kuhusu uamuzi wake wa kumchukua mtoto huyo na kumtunza kama mtoto wake mwenyewe.

"Nitaendelea kutafuta haki kwa niaba yake hadi wahalifu wote waliomuua mtu pekee ambaye alijua kama mzazi katika ulimwengu huu watakapopatikana. Roho ya baba yake ipumzike mahali pema peponi,” alisema.

 Marehemu Michael Oworo alidungwa kisu na kuuawa alipokuwa akimsindikiza mwanawe shuleni kwenye shambulizi katika mitaa ya mabanda ya Mathare, Nairobi.

 Wenyeji walisema walisikia kelele na vifijo mnamo Januari 20 asubuhi na walipofika eneo la tukio ili kujua chanzo, walipatana na mwili wa Michael Oworo ukiwa kwenye dimbwi la damu.

 Mwanawe alisimama mita chache huku akilia bila kujua nini cha kufanya baada ya mauaji ya baba yake.

 Polisi na wenyeji walisema mwathiriwa alikuwa akimpeleka mwanawe katika kituo cha kulea watoto katika eneo hilo wakati mshambuliaji alipomvamia.

 Michael alitaka kumpeleka mtoto huyo kituoni kisha kuelekea eneo la ujenzi ambako alifanya kazi ya uashi kwa ajili ya kujikimu.

 Sababu ya shambulio hilo bado haijajulikana lakini wenyeji walisema mauaji hayo yalitokea katika harakati za wizi.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved