
Papa Francis anaendelea kupata nafuu baada ya kuugua nimonia na
matatizo ya figo huku maombi ya usiku yakiendelea katika makao yake rasmi,
Vatican.
Waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki kote duniani wanaendelea kumuombea kiongozi huyo, wakitumai atapona haraka na kurejea katika majukumu yake ya kuongoza Kanisa Katoliki.
Taarifa ya kila asubuhi kutoka Vatican siku ya Jumanne ilisema, “Papa amelala vizuri usiku kucha.”
Licha ya kuwa katika hali tete kutokana na nimonia katika mapafu yote mawili, madaktari walisema Jumatatu jioni kwamba kulikuwa na “kuboreka kidogo” katika baadhi ya vipimo vya afya yake.
Aidha, iliripotiwa kuwa ameanza tena kazi zake akiwa hospitalini, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na parokia moja mjini Gaza, ambako amekuwa akifuatilia hali tangu vita vilipoanza.
Baada ya jua kutua Jumatatu, waumini kwa maelfu walikusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, licha ya mvua kubwa, kwa ibada ya Rosari iliyoanza rasmi kama sehemu ya maombi ya kila usiku kwa ajili ya Papa Francis.
Hali hii ilikuwa kukumbuka usiku wa maombi mwaka 2005 wakati Papa John Paul II alipokuwa katika siku zake za mwisho.
Kwenye madhabahu ambako Papa Francis huongoza ibada, Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, alihimiza waumini wote kushiriki kwa moyo mmoja katika sala kwa ajili ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.
"Kuanzia jioni hii, tunataka kuungana katika sala hii hapa, nyumbani kwake," alisema Parolin, akimuombea Papa ili apone haraka kutoka kwa “hali hii ya ugonjwa na majaribu.”
Papa Francis, ambaye alipoteza sehemu ya pafu lake akiwa kijana, amelazwa hospitalini tangu Februari 14.
Madaktari wanasema hali yake ni ya kutia wasiwasi kutokana na umri wake mkubwa na matatizo ya awali ya upumuaji.
Hata hivyo, ripoti za Jumatatu zilionyesha kuwa hakupata tatizo kubwa la upumuaji tangu Jumamosi, na kiwango cha oksijeni anachosaidiwa nacho kimepunguzwa kidogo.
Matatizo ya figo yaliyobainika Jumapili bado hayajaleta hofu kubwa kwa sasa, ingawa madaktari wanaendelea kumfuatilia kwa ukaribu.
Wakati huo huo, baadhi ya wakosoaji wake wa mrengo wa kulia wameeneza uvumi wa kutia shaka kuhusu hali yake, lakini wafuasi wake wameendelea kumtia moyo na kumuombea.
Wengi wamemkumbuka kwa unyenyekevu wake, hasa tangu siku ya kwanza alipochaguliwa kuwa Papa alipowaomba waumini wamuombee.
Waumini na viongozi wa Kanisa wanaendelea kumuombea Papa Francis, wakitumai kwamba atapata nafuu haraka na kurejea katika uongozi wa Kanisa Katoliki.