logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Hali ya Papa Francis yafichuliwa huku akimaliza siku 13 hospitalini

Papa Francis amelazwa kwa zaidi ya siku 13 katika Hospitali ya Gemelli ambako madaktari wanaendelea kufuatilia afya yake.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri27 February 2025 - 08:33

Muhtasari


  • Vatican imeeleza kuwa hali ya afya ya Papa Francis inaendelea kuimarika polepole, huku uchunguzi wa picha ukionyesha maendeleo mazuri.
  • Uchunguzi wa picha ya kifua umeonyesha maendeleo ya kawaida ya kupona kwa uvimbe katika mapafu yake.

Pope Francis /SCREENGRAB

Vatican imeeleza kuwa hali ya afya ya Papa Francis inaendelea kuimarika polepole, huku uchunguzi wa picha (CT scan) ukionyesha maendeleo mazuri katika mapafu yake.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumatano jioni, Februari 26, na Ofisi ya Habari ya Vatican, ilibainika kuwa matatizo madogo ya figo yalilogunduliwa siku chache zilizopita sasa yametoweka, ishara njema kwa afya ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.

"Hali ya Baba Mtakatifu imeonyesha kuimarika kidogo zaidi katika saa 24 zilizopita. Tatizo ndogo la figo liliobainika siku za hivi majuzi limepungua," ilisema taarifa hiyo.

Aidha, uchunguzi wa picha ya kifua uliofanywa usiku wa kuamkia Jumanne umeonyesha maendeleo ya kawaida ya kupona kwa uvimbe katika mapafu yake.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amelazwa kwa zaidi ya siku 13 katika Hospitali ya Gemelli, Rome, ambako madaktari wanaendelea kufuatilia afya yake kwa karibu. Japokuwa madaktari wake wanabaki na tahadhari katika tathmini yao, inaripotiwa kuwa anapata lishe vizuri na hata anatekeleza baadhi ya majukumu yake ya kikazi akiwa hospitalini.

Tangu alazwe tarehe 14 Februari 2025, Papa aligunduliwa kuwa na maambukizi ya mfumo wa kupumua pamoja na nimonia kwenye mapafu yote mawili.

Hali hii imechangiwa na historia yake ya kiafya, ambapo alipokuwa kijana alikumbwa na pleurisi na kulazimika kuondolewa sehemu ya pafu lake moja.

Waumini wa Kanisa Katoliki kote ulimwenguni wameendelea kumwombea Papa Francis. Ibada za maombi za kila usiku zinaendelea katika Basilika la Mtakatifu Petro, pamoja na maeneo mengine nchini Italia na nje ya nchi. Waumini pia wamekuwa wakikusanyika nje ya Hospitali ya Gemelli wakimwombea afya njema.

Hii si mara ya kwanza kwa Papa Francis kukumbwa na matatizo ya kiafya. Machi 2023, alilazwa hospitalini kwa nimonia, na Juni 2021, alifanyiwa upasuaji wa utumbo mpana. Kwa miaka ya hivi karibuni, amekuwa akionekana mara kwa mara akitumia kiti cha magurudumu au fimbo kutokana na matatizo ya neva ya sciatica na maumivu ya goti.

Licha ya changamoto za kiafya, Papa aliendelea na ratiba yake ngumu ya majukumu ya kidini hadi alipopatwa na hali iliyosababisha kulazwa kwake mwezi huu. Kwa sasa, madaktari wanaendelea kufuatilia afya yake kwa umakini huku ulimwengu wa Katoliki ukiendelea kumuombea afya njema na kupona haraka.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved