
Kiongozi wa kanisa la Katoliki Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, alikumbwa na matatizo makubwa ya upumuaji baada ya kupata vipindi viwili vya kushindwa kupumua siku ya Jumatatu, hali iliyosababishwa na mkusanyiko mkubwa wa kamasi kwenye njia za hewa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Vatican Jumatatu jioni, hali hiyo ilisababisha bronkospasmu (bronchospasm), yaani mishtuko ya ghafla kwenye mirija ya hewa, na hivyo kulazimu hatua za matibabu ya haraka.
"Leo, Baba Mtakatifu alipata vipindi viwili vya kushindwa kupumua vilivyosababishwa na mkusanyiko mkubwa wa kamasi kwenye mirija ya hewa, hali iliyopelekea bronkospasmu," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa sababu hiyo, madaktari walilazimika kufanya bronkoskopi mara mbili ili kuondoa kamasi hizo zilizokuwa zikizuia mfumo wa hewa wa Papa Francis.
Baada ya taratibu hizo, Papa aliwekwa tena kwenye mashine ya kusaidia upumuaji isiyoingilia mwili ili kupunguza athari za hali yake.
Taarifa ya Vatican imeeleza kuwa licha ya changamoto hizo, Papa Francis alibaki macho, mwenye fahamu, na mwenye kujibu wakati wote wa matibabu. Hata hivyo, madaktari wamesema hali yake bado ni ya tahadhari .
Vipimo vya damu vilivyochukuliwa Jumatatu vimeonyesha kuwa Papa hana ongezeko la chembe nyeupe za damu (leukocytosis), jambo linaloashiria kuwa hakuna maambukizi mapya. Madaktari wanaamini kuwa mkusanyiko wa kamasi ulitokana na nimonia aliyokuwa akiugua hapo awali.
Sababu kuu ya vipindi hivyo vya kushindwa kupumua ni mwitikio wa bronchi zake uliojumuisha kutanuka kwa njia ya hewa kwa lengo la kuondoa kamasi hizo.
Hata hivyo, badala ya kusaidia, hali hiyo ilisababisha kuziba kwa njia za hewa, hivyo kuathiri upumuaji wake. Kutokana na hali hii, Vatican imeonya kuwa kuna uwezekano wa vipindi vingine vya kushindwa kupumua kutokea tena.
Papa Francis amelazwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma tangu Februari 14 kutokana na matatizo ya upumuaji. Madaktari walithibitisha kuwa nimonia iliyoathiri mapafu yake yote mawili ilisababisha upungufu mkubwa wa oksijeni mwilini. Hii si mara ya kwanza kwa Papa Francisko kupata matatizo ya kiafya; hapo awali, alikuwa tayari ameondolewa sehemu ya pafu moja alipokuwa kijana kutokana na maambukizi ya mapafu.
Kwa sasa, shughuli nyingi za kipapa zimeahirishwa au kugawiwa kwa maafisa wengine wa Kanisa Katoliki. Kwa mfano, Kardinali Angelo De Donatis atamwakilisha Papa katika ibada ya Jumatano ya Majivu inayotarajiwa kufanyika Machi 5.
Waumini wa Kanisa Katoliki kote ulimwenguni wanaendelea kumuombea Papa Francisko apate nafuu haraka. Hali yake inaendelea kufuatiliwa kwa karibu na madaktari, huku Vatican ikisisitiza kwamba ingawa amepata nafuu kiasi, bado hali yake inahitaji uangalizi maalum ili kuepusha matatizo zaidi ya kiafya.