
Leo, Jumamosi, Machi 8, 2025, taifa la Kenya linaaga rasmi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Wanyonyi Chebukati, ambaye atapumzishwa katika shamba lake la Sabata, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.
Mwili wake uliwasili katika uwanja wa ndege wa Kitale Alhamisi jioni, Machi 6, 2025, ambapo ulipokelewa na familia, marafiki na viongozi wa kisiasa.
Mbunge wa Kwanza, Ferdinand Wanyonyi, ametoa wito kwa wakazi wa Trans Nzoia na Wakenya kwa jumla kujitokeza kwa wingi ili kutoa heshima za mwisho kwa Chebukati.
Akizungumza Alhamisi, siku mwili ulipowasili, Wanyonyi alisisitiza kuwa hafla hiyo inapaswa kuwa ya maombolezo pekee na si jukwaa la siasa.
"Tunaomboleza; hakuna shughuli nyingine. Sina tatizo na yeyote kuzungumza lakini siasa hapana; hakuwa mwanasiasa bali mtumishi wa umma. Tusubiri hadi 2027 kuzungumzia siasa," alisema.
Aidha, Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, alionya dhidi ya viongozi wanaoweza kutumia mazishi haya kwa maslahi yao ya kisiasa.
"Trans Nzoia si ugani wa Kaunti ya Bungoma. Tuna watu wetu Bungoma, na tunawapenda, lakini kuhusu masuala ya Trans Nzoia, tunapaswa kuachwa tuendeshe mambo yetu," Natembeya alisema
Chebukati aligunduliwa na saratani ya ubongo mwezi Aprili 2023, miezi michache baada ya kustaafu kutoka IEBC.
Alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa nchini Ujerumani na kurejea nchini Julai 2023 kuendelea na shughuli mbalimbali, ikiwemo kushiriki katika mikutano ya uchaguzi katika nchi za kigeni. Hata hivyo, hali yake ilizorota mapema 2025, na alifariki dunia Februari 20, 2025, akiwa na umri wa miaka 63, katika Hospitali ya Nairobi alipokuwa akipokea matibabu.
Chebukati alihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita, kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2023.
Katika kipindi chake, alisimamia chaguzi mbili kuu zilizokuwa na ushindani mkubwa na utata; uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 na ule wa 2022.
Ingawa alikumbana na changamoto nyingi, ikiwemo kujiuzulu kwa makamishna na shutuma za uongozi, alifanikiwa kukamilisha muhula wake na kustaafu Januari 17, 2023.
Mola ailaze roho ya Chebukati pema peponi!