Shirika la utangazaji nchini KBC limeamkia maombolezo kufuatia kifo cha Fredrick Parsayo, mwandishi wa habari ambaye amekuwa akihudumu katika kitengo cha uhariri.
Wasimamizi wa kitua hicho wametangaza kuwa marehemu alifariki Ijumaa, Machi 21, nyumbani kwake katika eneo la Kinoo, kaunti ya Kiambu.
Kulingana na shirika la habari, mwandishi huyo wa habari alikufa kwa njia isiyoeleweka na tayari maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo.
"Ni kwa moyo mzito kwamba tunatangaza habari za kifo cha mwenzetu mpendwa, Fredrick Parsayo ambaye amekuwa mwandishi wa habari katika Idara ya Wahariri ya KBC," sehemu ya taarifa ya KBC ilisoma.
Fredrick ametuacha kwa huzuni Ijumaa, Machi 21, 2025, chini ya hali ambazo bado zinachunguzwa, nyumbani kwake katika eneo bunge la Kinoo-Kikuyu. Jambo hili lisilotarajiwa limetuathiri sana sisi sote," taarifa hiyo iliongeza.
Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kinoo, na mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha St Teresa huku familia yake ikiwa tayari imearifiwa kuhusu kifo chake.
KBC imemtaja Fredrick mtu aliyejituma kwa kazi yake na kusaidia pakubwa kwenye kitengo cha uhariri kwenye shirika hilo la habari.
"Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya KBC, Usimamizi, na wafanyikazi wetu wote, tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia ya Fredrick, marafiki, na wale wote walioathiriwa na kifo chake," shirika la habari lilitangaza.