
Afisa wa polisi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru, amevuliwa silaha na kukamatwa baada ya kudaiwa kuhusika katika tukio la risasi dhidi ya mwendesha bodaboda Jumatano usiku.
Kwa mujibu wa ripoti za polisi, tukio hilo lilitokea baada ya mwendesha bodaboda huyo kumpeleka mke wa afisa huyo nyumbani usiku.
Mwendesha bodaboda huyo, anayejulikana kama Edwin Keitany, alipigwa risasi na kujeruhiwa na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa Jumamosi ili kuondoa vipande vya risasi vilivyobaki mwilini mwake, maafisa wamesema.
Huku akiwa hospitalini, mwathiriwa alitoa taarifa kwa Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA).
Kwa sasa, madaktari wa Hospitali ya Nairobi Women’s tawi la Nakuru wanamhudumia mwathiriwa huyo mwenye umri wa miaka 25.
Keitany alilazwa hospitalini hapo Alhamisi na kudai kuwa alipigwa risasi na kujeruhiwa na afisa wa polisi baada ya ugomvi kuzuka kati ya afisa huyo wa DCI na abiria wa kike anayedaiwa kuwa mke wake.
"Abiria huyo aliniomba nimpeleke kwake huko Ole Polos. Tulipofika, nilimkuta mwanamume akisubiri, akanijia juu na kuniuliza kwanini nilikuwa nimekuja na mke wake. Mvutano ulizuka, ghafla nikahisi maumivu na damu," alisimulia mwathiriwa.
Kwa sasa, mshukiwa, ambaye ana cheo cha Sajini, yuko rumande huku bastola yake yenye risasi 14 za milimita 9 ikiwa imechukuliwa kama ushahidi.
Daktari wa zamu alisema mwathiriwa amepata majeraha makubwa kwenye tishu laini, huku uchunguzi wa CT scan ukionyesha vipande vingi vya risasi kwenye sehemu ya mbele ya kichwa chake.
Tukio hili linajiri wakati visa vya maafisa wa polisi kujihusisha na ufyatuaji risasi vimeendelea kushuhudiwa.
Mnamo Machi 23, afisa wa polisi anayehudumu katika ofisi ya Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, alishukiwa kumuua mwanamume mmoja wakati wa ugomvi uliotokea Kawangware, Nairobi, kuhusu mchezo wa pool.
Mapema mwezi huo, afisa wa polisi wa Bunge alipiga risasi na kumuua mwenzake baada ya ugomvi kuhusu vyeo vyao na kumjeruhi mwingine katika kantini ya polisi Gigiri.
Katika tukio jingine mnamo Februari mwaka huu, afisa aliyekuwa kwenye kikosi cha ulinzi wa viongozi wakuu alipiga risasi na kumuua mwenzake aliyekuwa akihudumu katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) baada ya ugomvi eneo la Ruaraka. Alikamatwa baadaye.
Polisi wanasema wanachunguza matukio haya, wakisisitiza kuwa ni visa vya kipekee.
Visa vingi vya polisi kuhusika katika ufyatuaji risasi vimehusishwa na msongo wa mawazo kazini. Mamlaka zimeanzisha mipango maalum ya kushughulikia changamoto ya msongo wa mawazo kwa maafisa wa polisi.