logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mke wa afisa wa Kenya aliyetoweka Haiti afichua mazungumzo yao ya mwisho

Bi Miriam alifichua kuwa alizungumza na mumewe siku ya tukio la kushambuliwa na genge lililosababisha kupotea kwake.

image
na Samuel Mainajournalist

Makala29 March 2025 - 09:21

Muhtasari


  • Miriam alieleza mazungumzo yao ya mwisho, akisema mumewe alimwambia akachukue zawadi ya kushangaza aliyokuwa ameagiza kwa ajili yake.
  • Mama yake Benedict, Bi. Jacinta Wanjiru Kabiru, aliwataka wananchi kuacha kusambaza habari zisizo na ukweli kuhusu madai ya kifo cha mwanawe.

Bi Miriam Watima amefichua mazungumzo ya mwisho na mumewe, Benedict Kabiru

Familia ya afisa wa polisi wa Kenya aliyeripotiwa kutojulikana aliko kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea katika operesheni ya kulinda amani nchini Haiti, Benedict Kabiru, imevunja ukimya kuhusu kutoweka kwake..

Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, Machi 27, mke wa afisa huyo, Miriam Watima, alifichua kuwa alizungumza naye siku ya tukio la kushambuliwa na genge lililosababisha kupotea kwake.

Miriam alieleza mazungumzo yao ya mwisho, akisema mumewe alimwambia akachukue zawadi ya kushangaza aliyokuwa ameagiza kwa ajili yake.

 "Aliniambia, 'Kesho nenda uchukue kitu nimeitisha—ni surprise. Na usinipigie simu kesho ukiniambia hujaenda.' Nikamwambia nitaenda. Nilipomuuliza ni nini, akasema nisiwe na wasiwasi—ni zawadi yangu ya kushangaza," Miriam alisimulia.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema alishtuka sana kuona maafisa wengi wa polisi wakifika nyumbani kwao asubuhi iliyofuata kuwapa taarifa za kusikitisha.

"Nilipoamka asubuhi, maafisa wa polisi walikuja kwa wingi. Nikauliza kwa nini mmekuja kwa idadi hii kubwa na nikaomba waniambie ukweli—kama amefariki au la. Wakasema, 'Hapana, ametoweka,'" alisema.

Mama yake Benedict, Bi. Jacinta Wanjiru Kabiru, aliwataka wananchi kuacha kusambaza habari zisizo na ukweli kuhusu madai ya kifo cha mwanawe.

Wanjiru alitupilia mbali picha na video zinazosambaa mtandaoni zikionyesha mwili wake ukiwa amefariki, akidai kuwa zimechezewa. Alisisitiza kuwa anaamini mwanawe yuko hai.

"Ninaomba umma na mtu yeyote anayesambaza uvumi kuwa mwanangu amekufa, hata kuweka picha zake, aache. Sijamruhusu yeyote kuzungumza kuhusu kifo cha mwanangu kwa sababu najua na naamini kuwa bado yuko hai. Hajulikani aliko tu. Katika video, kuna picha mbili—moja akiwa amelala barabarani akipigwa, na nyingine. Ile ya kwanza uso ni wake, lakini hii nyingine inaweza kuwa imehaririwa kwa Photoshop," Bi. Wanjiru alisema.

 Miriam pia alieleza jinsi mumewe alivyompa moyo, akimwambia kuwa wana imani na ushindi wao katika operesheni hiyo.

"Mara zote alikuwa ananipa moyo, akiniambia mambo si mabaya jinsi yanavyoonekana. Alisema wao ni hodari na lazima wamnase huyo kiongozi wa genge. Aliniambia nisiwahi kuwa na wasiwasi. Hivi majuzi aliniambia kuwa walihamishiwa kambi nyingine," alisema.

Benedict, ambaye aliripotiwa kutoweka Machi 25, 2025, anatoka kaunti ndogo ya Kikuyu katika Kaunti ya Kiambu na amekuwa afisa wa usalama tangu mwaka 2015.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved