logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Polisi wavunja kimya baada ya afisa wa Kenya kutopatikana kufuatia uvamizi wa genge Haiti

Idara hiyo imesema inaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu, huku ikiwapongeza maafisa wote waliopo Haiti kwa ujasiri wao.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri26 March 2025 - 10:13

Muhtasari


  • NPS imethibitisha kuwa afisa huyo alitoweka mnamo Machi 25, 2025, kufuatia shambulio la kushtukiza karibu na barabara ya Carrefour Paye-Savien.
  • “Tunawapongeza maafisa wetu wanaoendelea kutoa huduma Haiti, licha ya changamoto. Tumejizatiti kuhakikisha usalama wao," NPS imesema.

Kenyan police officers arriving in Haiti

Idara ya Huduma kwa Polisi ya Kenya (NPS) imevunja ukimya baada ya kuthibitisha kutoweka kwa afisa wake mmoja anayehudumu katika Mpango wa Usalama wa Kimataifa nchini Haiti (Multinational Security Support Mission – MSS).

Katika taarifa yake ya Jumatano asubuhi, NPS ilithibitisha kuwa afisa huyo alitoweka mnamo Machi 25, 2025, kufuatia shambulio la kushtukiza karibu na barabara ya Carrefour Paye-Savien, eneo la Pont-Sonde, Mkoa wa Artibonite.

“Tumepokea taarifa kwamba afisa wa Polisi wa Kenya anayehudumu chini ya Mpango wa Usalama wa Kimataifa nchini Haiti amepotea,” ilisema sehemu ya taarifa rasmi lililotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Msemaji wa Idara ya Huduma kwa Polisi, Bw. Muchiri Nyaga.

Kulingana na taarifa hiyo, kikosi cha MSS, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi la Haiti (HNP), kinafanya juhudi za haraka za utafutaji na uokoaji ili kubaini alipo afisa huyo.

Idara hiyo imeeleza kuwa inaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu, huku ikiwapongeza maafisa wote waliopo Haiti kwa ujasiri wao katika kutekeleza majukumu yao.

“Tunawapongeza maafisa wetu wanaoendelea kutoa huduma nchini Haiti, licha ya changamoto. Tumejizatiti kuhakikisha usalama wao na tunashirikiana kikamilifu na mamlaka za Haiti,” ameongeza Bw. Nyaga.

Taarifa hiyo pia  inasisitiza kwamba Jeshi la Polisi la Kenya linaendelea kuheshimu na kutimiza wajibu wake katika Mpango wa Usalama wa Kimataifa.

Aidha, polisi wametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kumpata afisa huyo kujitokeza na kushirikiana na vyombo vya usalama.

Pia wameomba umma na vyombo vya habari kuwa watulivu wakati uchunguzi na operesheni za kumtafuta afisa huyo zinaendelea, likiahidi kutoa taarifa za ziada pindi tu zinapopatikana.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, Machi 25, 2025, na msemaji wa MSS, Jack Ombaka, shambulio lilitokea mwendo wa saa nne unusu jioni ya Jumatatu katika eneo la Pont-Sonde, jimbo la Artibonite, wakati gari la kivita la Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) lilipokwama kwenye mtaro unaoshukiwa kuchimbwa kwa makusudi na magenge ya wahalifu.

“Tulipopokea taarifa za tukio hilo, magari mawili ya kivita ya MSS Mine-Resistant Ambush Protected (MRAP) yalitumwa kutoka Pont-Sonde kusaidia katika operesheni ya uokoaji,” taarifa hiyo ilieleza.

Hata hivyo, juhudi za kuwaokoa maafisa wa Haiti zilitatizika baada ya moja ya magari ya MSS pia kukwama, huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi. Wakati vikosi vya uokoaji vikiendelea kushughulikia hali hiyo, washukiwa wa magenge waliokuwa wamejificha walitekeleza shambulio la kushtukiza.

Kufuatia mashambulizi hayo, afisa mmoja wa Kenya anayehudumu chini ya MSS bado hajapatikana. Ombaka alisema vikosi maalum vimeanzisha msako ili kubaini aliko.

“Kufuatia tukio hili, afisa mmoja wa Kikosi cha Kenya hajulikani aliko. Timu maalum za utafutaji na uokoaji zimepelekwa kufuatilia nyayo zake na kubaini alipo,” alisema msemaji wa MSS, Jack Ombaka.

MSS iliahidi kutoa taarifa ya kina baadaye kuhusu tukio hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved