logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Familia ya afisa wa Kenya aliyetoweka Haiti yavunja kimya kuhusu picha zinazoonyesha amefariki

Familia ya afisa Benedict Kabiru imezungumzia kutoweka kwake na madai ya kifo chake.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri29 March 2025 - 10:18

Muhtasari


  •  Akizungumza na wanahabari, mamake Kabiru, Jacinta Wanjiru, alikanusha madai kwamba mwanawe ameuawa, akisisitiza kuwa bado yu hai.
  • Wanjiru alikiri ameona picha na video zinazosambaa mitandaoni zikidai kuonyesha mwili wa mwanawe, lakini alizitaja kuwa zimekarabatiwa.

Bi Jacinta Wanjiru amezungumzia madai ya kifo cha mwanawe Benedict Kabiru

Familia ya Benedict Kabiru, afisa wa polisi wa Kenya anayehudumu katika operesheni ya kulinda amani nchini Haiti, imezungumzia kutoweka kwake na madai ya kifo chake..

 Akizungumza na wanahabari mnamo Machi 27, mama yake Kabiru, Jacinta Wanjiru Kabiru, alikanusha madai kwamba mwanawe ameuawa, akisisitiza kuwa bado yu hai.

 Bi Wanjiru alikiri kuwa ameona picha na video zinazosambaa mitandaoni zikidai kuonyesha mwili wa mwanawe, lakini alizitaja kuwa zimekarabatiwa.

Kutokana na hayo, alitoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa zisizothibitishwa kuhusu kifo cha mwanawe, ambaye anaamini bado anatafutwa. 

"Ninaomba umma pamoja na mtu anayesambaza uvumi kwamba mwanangu amefariki, hata kuposti picha zake—sijamruhusu mtu yeyote kuzungumzia kifo cha mwanangu. Kwa sababu najua na naamini, mwanangu yuko hai. Amepotea tu," Bi Wanjiru alisisitiza.

Aliongeza kuwa picha hizo zina utata. "Kwenye video, kuna picha mbili—moja anaonekana amelala barabarani akipigwa na nyingine. Katika moja, uso ni wake, lakini hii nyingine inaweza kuwa imechezewa kwa Photoshop," alisema.

Afisa Benedict Kabiru aliripotiwa kutoweka mnamo Machi 25, 2025, baada ya shambulio la genge wakati wa operesheni ya kulinda amani nchini Haiti. 

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, Machi 25, 2025, na msemaji wa Mpango wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa (MSS) Jack Ombaka, shambulio hilo lilitokea mnamo saa nne unusu jioni katika eneo la Pont-Sonde, jimbo la Artibonite, wakati gari la kivita la Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) lilipokwama kwenye mtaro unaoshukiwa kuchimbwa kwa makusudi na magenge ya wahalifu.

 “Tulipopokea taarifa za tukio hilo, magari mawili ya kivita ya MSS Mine-Resistant Ambush Protected (MRAP) yalitumwa kutoka Pont-Sonde kusaidia katika operesheni ya uokoaji,” taarifa hiyo ilieleza.

 Hata hivyo, juhudi za kuwaokoa maafisa wa Haiti zilitatizika baada ya moja ya magari ya MSS pia kukwama, huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi. Wakati vikosi vya uokoaji vikiendelea kushughulikia hali hiyo, washukiwa wa magenge waliokuwa wamejificha walitekeleza shambulio la kushtukiza.

 Kufuatia mashambulizi hayo, afisa wa Kenya Benedict Kabiru alitowekana na Ombaka alisema vikosi maalum vilikuwa vimeanzisha msako ili kubaini aliko.

 “Kufuatia tukio hili, afisa mmoja wa Kikosi cha Kenya hajulikani aliko. Timu maalum za utafutaji na uokoaji zimepelekwa kufuatilia nyayo zake na kubaini alipo,” alisema msemaji wa MSS, Jack Ombaka.

 MSS iliahidi kutoa taarifa ya kina baadaye kuhusu tukio hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved