
Kwa mara ya kwanza Rais William Ruto ameelezea vita vivyokuwepo kati ya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gchagua na maafisa wa kila ngazi katika serikali.
Katika mazungumzo ya moja kwa moja na vyombo vya habari vya Mlima Kenya Jumatatu jioni Rais alidai kuwa Gachagua alikuwa amekosana na karibu kila mtu akiwemo hata msaidizi wake Farouk Kibet.
“Kila siku kesi, mara Itumbi huyu blogger mdogo eti ameandika hii, siku ingine mara Farouk msaidizi wangu mtu wa chini...kesi ingine Kimani Ichung’wa mara amefanya nini,” Rais alisema.
Ruto aliendelea kusema kuwa Gachagua hakuwa na heshima kwa wafanyikazi wengine akidai kuwa kuna siku aliambia kiongozi mmoja wa kike kutoka Mt. Kenya kwamba kazi yake ilikuwa kuzungusha ‘marinda’.
“Kuna mama kiongozi hapa alisema wewe unazungusha marinda”, Rais aliongeza.
Rais Ruto alidai kuwa Gachagua pia alimtishia kwamba angemfanya rais wa mhula mmoja na kumhadaa ampe shilingi bilioni 10 ili kumsaidia kulainisha eneo la Mlima Kenya.
"Niliketi na Gachagua na kumwambia rafiki yangu acha vita hivi. Alinijia na kusema atanifanya rais wa mhula mmoja na akaomba Shilingi bilioni 10 ili niandae Mlima Kenya," Ruto alisema.
Alisema kuondolewa kwa Gachagua afisini ulikuwa uamuzi uliofanywa na wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya.
“Waliomuondoa walifuata sheria, sikuwahi kutia saini popote kwamba aondolewe afisini,” Ruto alisema.
Rais alisema kwamba Gachagua alikuwa amewatishia wabunge kuwa... “Msiponipigia magoti mtaenda nyumbani”...matamshi ambayo anasema yaliwakera sana wabunge na wakaazimia kumuondoa ofisi.