logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ruto akiwapa pesa, mzichukue - Gachagua awaambia wakazi wa Mt Kenya

Gachagua amewahimiza wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuhudhuria kwa wingi ziara ya Rais William Ruto.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri30 March 2025 - 08:25

Muhtasari


  • Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya maendeleo katika eneo hilo kuanzia Aprili 1, hatua inayotazamwa kama juhudi za kuimarisha uungwaji wake.
  • “Rais anakuja na zawadi, na nawahimiza mpokee kwa furaha,” alisema. 

Rigathi Gachagua akizunguza mnamo Machi 29, 2025

Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua amewahimiza wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuhudhuria kwa wingi ziara ya Rais William Ruto inayotarajiwa kuanza ndani ya siku tatu.

Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya maendeleo katika eneo hilo kuanzia Aprili 1, hatua inayotazamwa kama juhudi za kuimarisha uungwaji wake wa mkono baada ya mvutano wa kisiasa kati yake na Gachagua.

Akizungumza mjini Naivasha siku ya Jumamosi, Gachagua aliwashauri wakazi wasisite kuhudhuria mikutano ya Rais. Aidha, alidokeza kuwa ikiwa waandalizi wa mikutano hiyo watawapa fedha kama motisha, basi wakazi wakubali bila kusita.

“Rais anakuja na zawadi, na nawahimiza mpokee kwa furaha,” alisema.

“Kama wanawapa pesa, ombeni zaidi. Msikubali kiasi kidogo.”

Aliongeza, “Rais Ruto, jiandae kifedha kwa sababu tulikuchagua bila kudai chochote.”

Gachagua alitoa matamshi haya wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Mchungaji Harrison Munyua katika Kanisa la Redeemed mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru. Alipokuwa mjini humo, alisimama kuwasalimia wakazi na kuwashukuru: "Asanteni sana watu wa Naivasha!"

Pia alitumia fursa hiyo kujibu matamshi ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Charles Kahariri kuhusu kaulimbiu za kisiasa. Akizungumza katika mhadhara wa umma katika Chuo cha Kitaifa cha Ujasusi na Utafiti (NIRU) siku ya Alhamisi, Jenerali Kahariri alionya dhidi ya matumizi ya kaulimbiu zinazohamasisha kuondolewa kwa viongozi kinyume cha katiba, akisema jeshi halitaruhusu vitendo vinavyovuruga demokrasia.

“Hatuwezi kuwa na vurugu kama taifa,” alisema Jenerali Kahariri. “Hata watu wanapotekeleza uhuru wao, lazima wafanye hivyo ndani ya mipaka fulani. Mlichagua serikali, na ikiwa hamridhiki, mabadiliko lazima yafanywe kwa njia ya kikatiba.” 

Hata hivyo, Gachagua alitetea kaulimbiu hizo, akisema ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Pia alionya polisi dhidi ya kuingilia mikutano ya kisiasa ambako wananchi wanatumia haki yao ya kidemokrasia kupinga sera zisizopendwa, akisema enzi ya kutumia polisi kudhibiti siasa imepitwa na wakati. 

Wakati huo huo, ratiba ya ziara ya Rais Ruto inaonyesha kuwa ataanza ziara yake katika Kaunti ya Laikipia mnamo Aprili 1, kisha ataelekea Meru, Kirinyaga, Nyandarua, Murang’a, Tharaka Nithi na Embu. Anatarajiwa kumaliza ziara yake Nyeri na Kiambu mnamo Aprili 5.

Kabla ya kuwasili kwake, viongozi wakuu wanaomuunga mkono, akiwemo Naibu wake Kithure Kindiki na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, wamekuwa wakizunguka eneo la Mlima Kenya kuhamasisha na kuweka mazingira tayari kwa ziara hiyo.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved