
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amekanusha madai kwamba alijaribu kumshawishi Rais William Ruto kwa kumtaka ampe Shilingi bilioni 10.
Madai hayo yaliibuka mwezi Machi wakati Rais Ruto, katika mahojiano na vyombo vya habari mjini Nyeri, alidai kwamba Gachagua alimtaka kiasi hicho cha fedha ili kusaidia kuimarisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya.
Hata hivyo, Gachagua, akizungumza kwenye mahojiano ya runinga ya KTN Jumatatu jioni, alikanusha vikali madai hayo, akisisitiza kwamba ana mali za kutosha na hahitaji fedha kutoka kwa Rais.
“Rais hakuzungumza kuhusu madai ya kunishinikiza hadi alipofika Mlima Kenya,” alisema Gachagua. “Kama kweli ningemshinikiza, hilo lingekuwa shtaka la kwanza katika hoja ya kuniondoa madarakani Bungeni—halikuwepo. Kumlazimisha mtu ni kosa la jinai,” Gachagua alisema.
Gachagua aliongeza kuwa wakati Ruto alitembelea eneo la Magharibi mwa Kenya, alihusisha kutofautiana kwao na masuala ya kutojali na ukabila, si kwa madai ya rushwa.
“Alipokuwa Magharibi, alisema aliniachisha kazi kwa sababu mimi si mweledi na ni wa kikabila. Hakuwambia kwamba nilimtaka Shilingi bilioni 10,” alisema.
Akijitetea kuhusu hali yake ya kifedha, Gachagua alisema amejijengea utajiri wake kupitia biashara nyingi kwa miaka mingi, na hahitaji msaada wa kifedha kutoka kwa mtu yeyote.
“Mimi si mtu wa kumwomba Rais pesa, na yeye anajua hilo. Mimi ni mfanyabiashara hodari ambaye nimefanya kazi kwa miaka mingi. Nilijiunga na kampeni kwa hiari yangu. Hakunilazimisha. Nilitumia pesa zangu kwa sababu niliamini katika jambo hilo. Pia nilisaidiwa na marafiki,” alieleza.
Alisisitiza kuwa kama kweli alitoa ombi hilo, Rais angekuwa amelizungumza miezi sita iliyopita.
Kauli za Gachagua zinakuja siku chache baada ya Rais Ruto kukamilisha ziara ya maendeleo ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya.
Wakati wa mahojiano yake mjini Nyeri, Ruto alidai kuwa Gachagua alimkabili moja kwa moja na kutoa sharti gumu.
“Niliketi na Gachagua nikamwambia, ‘Rafiki yangu, acha hizi
vita.’ Akaniambia kuwa nisipompa Shilingi bilioni 10, angenifanya kuwa rais wa
muhula mmoja kwa kuharibu uungwaji mkono wangu Mlima Kenya,” alisema Ruto.