
WATU wasiojulikana walitatiza kwa muda
ibada ya kanisa iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo
Aprili 6, 2025.
Kundi la vijana lilijaribu kuvamia ibada
katika Kanisa la PCEA Mwiki eneo bunge la Kasarani, na kuhatarisha usalama wa
waumini kwa muda.
Fujo hiyo ilitokea punde tu baada ya
Gachagua na msafara wake kufika kwa ibada ya Jumapili.
Katika video zilizoenezwa mitandaoni
Jumapili mchana, makumi ya vijana walionekana kuingia katika kanisa hilo kwa
fujo na kuwalazimu waumini kukimbilia usalama wao.
Iliwabidi walinzi wa Gachagua kufyatua
risasi hewani kuwatawanya watu huku mali kadhaa zikiharibiwa yakiwemo magari.
Wakati wa mvutano huo, gari la Gachagua
lilipigwa mawe, na madirisha kuvunjwa, kulingana na picha na video
zilizoonekana mitandaoni.
Mpaka wakati wa kuchapishwa kwa ripoti hii,
haijulikani kundi hilo la vijana walikuwa wanalenga nini wakati wa kuvamia
mkutano huo wa ibada.
Uvamizi huu unajiri siku moja tu baada ya rais William Ruto kukamilisha iara yake ya wiki moja katika eneo la Mlima Kenya.