logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Nalilia Kenya! Gachagua apinga kauli za Ruto, amuita muongo sugu

Ruto alimshtumu Gachagua kwa kufanya makosa makubwa matatu, ikiwa ni pamoja na kuwatisha wabunge wa Mlima Kenya.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri01 April 2025 - 07:24

Muhtasari


  • Gachagua, anaonekana kutoridhishwa na matamshi ya Rais William Ruto wakati wa mahojiano na vituo vya habari vya Mlima Kenya Jumatatu jioni.
  • "Wale waliomwondoa walifuata sheria. Sikuwahi kusaini popote kwa ajili ya kuondolewa kwake," Ruto alisema.

Rigathi Gachagua amemshtumu rais William Ruto kwa kuwa muongo

Makamu wa Rais wa zamani, Rigathi Gachagua, anaonekana kutoridhishwa na matamshi ya Rais William Ruto wakati wa mahojiano na vituo vya habari vya Mlima Kenya Jumatatu jioni.

Baada ya mahojiano hayo, Gachagua alituma ujumbe kwenye mitandao yake ya kijamii, akionekana kumshutumu rais kwa kuwa mwongo sugu—tabia anayoamini kuwa tishio kubwa kwa taifa.

"Sasa ninaamini zaidi ya hapo awali kwamba uongo wa mara kwa mara ni ugonjwa wa akili. Tishio kubwa zaidi kwa taifa letu pendwa ni uongo wa wazi kwa Wakenya bila kusita, na kushindwa kwa kiongozi kuunganisha timu yake ili kuweka uongo wao sawa. Nalia kwa ajili ya nchi yangu, Kenya,” Gachagua aliandika kwenye X.

Katika mahojiano hayo, ambayo yalifanyika kabla ya ziara yake ya siku tano Mlima Kenya, Rais Ruto alifafanua kuhusu mvutano wake na Gachagua, akimtuhumu kwa vitisho na ulaghai. Ruto alidai kuwa Gachagua alidai KSh10 bilioni ili kusaidia kupata uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya, akimtishia kumfanya kuwa rais wa muhula mmoja endapo angekataa.

"Nilikaa chini na Gachagua nikamwambia, rafiki yangu, acha hizi vita. Alikuja kwangu na kuniambia angenifanya rais wa muhula mmoja isipokuwa nimpe KSh10 bilioni ili kuandaa Mlima Kenya kwa ajili yangu," Ruto alidai.

Ruto alieleza zaidi kuwa wabunge wa Mlima Kenya walimkataa Gachagua tangu mwanzo alipotafutwa kama mgombea mwenza mnamo 2022. Kulingana naye, uamuzi wa kumwondoa Gachagua haukuwa wake peke yake bali ulifanywa na wanasiasa wa Mlima Kenya kwa kufuata taratibu za kisheria.

"Wale waliomwondoa walifuata sheria. Sikuwahi kusaini popote kwa ajili ya kuondolewa kwake," Ruto alisema.

Alisimulia kuwa wakati wa kuchagua mgombea mwenza, aliwashauri viongozi wa Mlima Kenya na kuwaomba wampendekeze mmoja wao. Hata hivyo, baada ya mkutano wa siku nzima katika makazi yake ya Karen wakati huo, viongozi hao walishindwa kufikia mwafaka na wakaamua kupiga kura.

"Katika kura hiyo, Kindiki alipata kura 27, huku rafiki yangu Rigathi akipata kura tano pekee," Ruto alifichua.

Licha ya hayo, Ruto alisema alitumia mamlaka yake na kumchagua Gachagua kama mgombea mwenza, akieleza kuwa alitaka mtu wa karibu na umri wake ili kukanusha madai kuwa alikuwa akipendelea viongozi wachanga wa Mlima Kenya.

Baada ya kushika madaraka, Ruto alimtuhumu Gachagua kwa kufanya makosa makubwa matatu, ikiwa ni pamoja na kuwatisha wabunge wa Mlima Kenya.

"Kila siku kulikuwa na malalamiko kuhusu watu aliokuwa akiwalenga, akiwemo Dennis Itumbi, Farouk Kibet, Ndindi Nyoro, na Kimani Ichung’wah," Ruto alisema. "Nilikaa naye chini na kumwambia aache, lakini alisisitiza kuwa wabunge ambao hawatamuunga mkono na kumpigia magoti wangekuwa nyumbani ifikapo Desemba."

Kulingana na Ruto, sababu nyingine ya kumwondoa Gachagua ilikuwa kushindwa kwake kutetea au kueleza miradi ya serikali kwa umma.

"Nilipokuwa makamu wa rais, nilihudhuria mahojiano mengi zaidi kwenye runinga kuliko hata Rais Uhuru Kenyatta. Ilikuwa jukumu langu kutangaza miradi ya serikali. Je, ulimwona Rigathi kwenye runinga yoyote akizungumzia mipango ya serikali? Hapana," Ruto alisema.

Alisisitiza kuwa hakuna uamuzi uliofanywa serikalini bila kupitishwa na makamu wa rais, ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa miradi ya maendeleo, akidokeza kuwa Gachagua alishindwa kutekeleza wajibu wake.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved