Mwanariadha wa Marekani Sha'Carri Richardson atakosa Olimpiki ya Tokyo kwasababu alithibitishwa kutumia bangi wakati wa majaribio ya mbio hizo Marekani ili kuweza kuiwakilisha nchi.
Huku bangi ikiwa imehalalishwa katika majimbo mengi kote Marekani, kwanini bado imepigwa marufuku katika michezo?
Pamoja na nywele zake za rangi ya machungwa, tabasamu lake la kupendeza na kasi kama umeme, Sha'Carri Richardson hakuwa akikosa wakati wa mchujo wa kuelekea Michezo ya Olimpiki.
Alichukuliwa kama mwanamke wa sita mwenye kasi zaidi katika historia, na muda mzuri mno katika mbio za mita 100 wa 10.72, mkimbiaji wa Texas alitarajiwa kuwa mshindani mkuu wa medali ya dhahabu huko Tokyo.
Lakini wakati wachezaji wenzake watakapokuwa kwenye mbio hizo za wanawake za mita 100 siku ya Alhamisi, hatakuwapo.
Mwanzoni mwa Julai, ilitangazwa kwamba Bi. Richardson hangewakilisha Marekani kwenye michezo hiyo kwasababu baada ya kufanyiwa vipimo, alipatikana kuwa mtumiaji wa bangi wakati wa mbio za kufuzu.
Kama adhabu, Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya limempiga marufuku kushindana kwa mwezi mmoja na kufutilia mbali ushindi wake.
Ingawa marufuku ya siku 30 yalimalizika wakati michezo ya Tokyo imeanza, wanariadha wa Merekani walichagua kutomjumuisha kwenye timu.
Kuondolewa kwake katika mashindano hayo, kumesababisha mjadala mkali juu ya kukatazwa kwa matumizi ya bangi katika michezo ya Olimpiki.
Kwa kuzingatia kuwa bado bangi ni halali katika majimbo mengi ya Merekani, wengi wanashangaa kwanini bangi inapaswa kuendelea kupigwa marufuku.
Bangi inaongeza utendaji zaidi
Bangi imepigwa marufuku na Shirika la Kupambana na dawa za kusisimua misuli Duniani (Wada) tangu shirika hilo lilipounda orodha yake ya kwanza ya vitu vilivyokatazwa mnamo mwaka 2004.
Vitu kwenye orodha hiyo vinakidhi vigezo viwili kati ya vitatu:
1: Kudhuru afya ya mwanariadha
2: Kuongeza utendaji
3: Ni kinyume na nia ya michezo
Kigezo cha pili ndicho ambacho watu wanaonekana kukichukulia kwa uzito zaidi linapokuja suala la bangi, na imekuwa mada ya vipindi vingi.
Mnamo mwaka wa 2011, Wada ilitetea marufuku ya bangi kwenye ripoti iliyochapishwa katika jarida la Sports Medicine.
Lilinukuu utafiti juu ya uwezo wa bangi kupunguza wasiwasi, na Wada ikagundua kuwa bangi inaweza kusaidia wanariadha "kufanya vizuri zaidi wakiwa chini ya shinikizo na kupunguza msongo wa mawazo kabla na wakati wa mashindano."
Lakini matokeo hayo hayatoshi kuhitimisha kwamba bangi ni dawa ya kuongeza nguvu, anasema Alain Steve Comtois, mkurugenzi wa idara ya sayansi ya michezo katika Chuo Kikuu cha Quebec huko Montreal.
"Lazima uangalie suala hili kwa upana zaidi", anaiambia BBC.
"Ndio, viwango vya wasiwasi hupungua, lakini kwa data halisi ya kisaikolojia, inaonesha kuwa utendaji umepunguzwa".
Bwana Comtois alikuwa mmoja wa waandishi wa Jarida la Sports Medicine and Physical Fitness mwaka 2021 wakati wa mapitio ya utafiti juu ya utumiaji wa bangi kabla ya mazoezi na uwezo wake wa kuongeza utendaji kwa mwanariadha.
Jarida hilo liligundua kuwa utafiti mwingi unaelezea bangi kama inayozuia majibu ya kisaikolojia muhimu kwa utendaji mzuri, kwa kuongeza shinikizo la damu na kupunguza nguvu na usawa.
Jarida hilo halikuangazia athari za bangi kwenye wasiwasi, lakini Bwana Comtois anasema athari zake zingine hasi zitapinga faida yoyote, ikitoa wazo kwamba bangi inaweza kuongeza utendaji wa riadha.
Dawa za kulevya na ari ya michezo
Lakini kuna zaidi ya sheria ya Wada ya kupiga marufuku dawa za kuongeza kusisimua misuli.
Sheria hiyo ilianzishwa mnamo mwaka 1999 baada ya kashfa kadhaa maarufu za utumiaji wa dawa za kulevya kwenye Olimpiki, Wada ikilenga kuongeza malipo ili kumaliza utumiaji wa dawa za kulevya katika michezo kote ulimwenguni.
Katika orodha yake ya vitu vilivyopigwa marufuku mnamo mwaka 2004, bangi ilikuwa haramu karibu katika kila nchi ulimwenguni.
"Hawakutaka kutokee shida katika suala la heshima kwenye jamii", anasema John Hoberman, mwanahistoria wa kitamaduni ambaye anachunguza historia ya kupambana na dawa za kulevya katika Chuo Kikuu cha Texas-Austin.
Hali yake kama dawa haramu ilinukuliwa na Wada katika jarida la 2011 kama moja ya sababu kwa nini bangi ilikosea "ari ya michezo", (kigezo 3) na"haiendani na mwanariadha kama mfano wa kuigwa kwa vijana ulimwenguni kote".
Sheria hiyo imesababisha kukemewa sio tu kwasababu ya Bi. Richardson, lakini pia hasara kwa wanariadha wengine kadhaa.
Mnamo 2009, Michael Phelps alipigwa marufuku kushindana kwa miezi mitatu, na alipoteza udhamini wa Kellogg, baada ya picha za yeye kuvuta bangi kuvuja mtandaoni.
Mwanariadha wa Marekani John Capel alipigwa marufuku kwa miaka miwili baada ya kupimwa kwa mara ya pili mnamo 2006 na kuthibitishwa kuwa mtumiaji wa bangi.
Kabla ya Wada kuunda orodha ya dawa za kulevya zilizokatazwa, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa ilijaribu kuchukua medali ya dhahabu ya mchezaji wa kutembea kwa ubao kwenye theluji wa Canada, Ross Rebagliati kwasababu hiyo hiyo.
Ilirejeshwa baada ya mahakama kuamuru kuwa hakuna sheria rasmi dhidi yake - IOC ilipiga marufuku matumizi ya bangi miezi miwili baadaye.
Kwa nini nchi nyingi sasa zinaruhusu matumizi ya bangi?
Lakini kwa muongo mmoja uliopita, hadhi ya kisheria ya bangi - na mtazamo wa jamii juu yake - imeanza kubadilika.
Uruguay ilikuwa ya kwanza kuhalalisha kisheria kununua na kuuza bangi kwa matumizi ya burudani mnamo mwaka 2013, na Canada ilifuata hatua hiyo mnamo 2018. Nchi nyingi zaidi zimehalalisha matumizi yake kwa kiwango fulani, pamoja na Afrika Kusini, Australia, Uhispania na Uholanzi.
Nchini Marekani, ni haramu kwa serikali kuu lakini ni halali katika karibu theluthi moja ya majimbo - pamoja na jimbo la Oregon ambapo Bi. Richardson alithibitishwa kuwa mtumizi.
Kumekuwa na ongezeko la kukubalika kwa matumizi ya bangi kwa madhumuni ya matibabu huku nchi nyingi, pamoja na Uingereza ikiruhusu bangi Kwa ajili ya matibabu.
Ukweli ni kwamba mnamo mwaka 2019, Wada iliondoa cannabidiol (CBD), sehemu ya bangi, kutoka kwenye orodha iliyopigwa marufuku, ingawa kemikali hiyo inabaki kuwa haramu katika nchi zingine kama Japani, ambapo mashindano ya Olimpiki yanafanyika mwaka huu.
Mabadiliko haya yamechochea ukosoaji wa sasa wa marufuku ya Bi Richardson.
Mkimbiaji huyo aliiambia NBC News kwamba alikuwa ametumia bangi kukabiliana na kifo cha mama yake wiki moja kabla ya mashindano ya mchujo.
"Ninaomba msamaha sana ikiwa nimewakatisha tamaa - na najua nimewatenda hivyo. Hii itakuwa mara ya mwisho Marekani kurudi nyumbani bila dhahabu katika mbio za mita 100", alisema.
Katikati ya huruma kwa Bi Richardson, Wada alikabiliwa na wakati mgumu.
Kama Bwana Hoberman anavyosema: "Huwezi kuendesha shirika ambalo lina sheria na ghafla ukazifuta kwa wakati unaotaka wewe."
Kwa sababu marufuku ya bangi bado iko kwenye vitabu, ubaguzi hauwezi kufanywa kwa kumpendelea Bi. Richardson.
Nini kinafuata?
Haijulikani ikiwa Wada itazingatia tena au lini kuhusu marufuku ya bangi lakini shinikizo linazidi kuongezeka.
Kupigwa marufuku kwa Bi. Richardson kulisababisha Rais Joe Biden wa Marekani kuhoji sheria ya sasa, ingawa hakukubali kusema inapaswa kubatilishwa, na kusababisha uvumi kwamba Ikulu inaweza kuingilia kati.
"Sheria ni sheria. Kila mtu anajua sheria zilizopo", Biden aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi huko Michigan.
"Ikiwa zinapaswa kusalia hivyo, ikiwa hiyo inapaswa kubaki kuwa sheria, hilo ni suala tofauti."
Hata Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya la Merekani, mamlaka ya Marekani inayosimamia sheria za Wada, ilisema "ni wakati wa kupitia tena suala hilo."
Hadi wakati huo, Bi. Richardson, na wanariadha wengine kama yeye, watalazimika kutokaribia bangi, au kukaa pembeni wakati wa mashindano ya mchezo huo.