Sadio Mane aondoka Bayern Munich kujiunga na Ronaldo Al-Nassr

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alifunga mabao 12 katika mechi 38 alizoichezea Bayern

Muhtasari

•Mapema Jumanne meneja wa Bayern Thomas Tuchel alisema yeye na Mane walikubaliana "ilikuwa uamuzi bora zaidi kuhama".

• Al-Nassr walimsajili Ronaldo mshindi mara tano wa Ballon d'Or mwezi Desemba na wamefuata mtindo huo msimu huu kwa kusajili wachezaji mahiri. 

Sadio Mane
Sadio Mane
Image: BBC

Mshambulizi wa zamani wa Liverpool Sadio Mane ameondoka Bayern Munich kujiunga na Cristiano Ronaldo katika klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alifunga mabao 12 katika mechi 38 alizoichezea Bayern katika msimu ambao haukuwa na matokeo ya kuridhisha licha ya awali kuonyesha kiwango kizuri cha mchezo.

Mchezaji huyo wa Senegal pia alihusika katika ugomvi wa kimwili na Leroy Sane katika chumba cha kubadilishia nguo cha Manchester City baada ya kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

Ripoti zinaonyesha kuwa mabingwa hao wa Ujerumani wamerudishiwa sehemu kubwa ya pauni milioni 35 walizolipa Liverpool kwa Mane mwaka mmoja uliopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern, Jan-Christian Dreesen alisema mchezaji huyo wa zamani wa Southampton - ambaye amesaini mkataba wa miaka minne na Al-Nassr – "hakuwa na msimu rahisi" tangu kuhama kutoka Anfield.

"Hakuwa na uwezo wa kuchangia kama sisi sote na yeye mwenyewe kama alivyotarajia," alisema Dreesen.

Mapema Jumanne meneja wa Bayern Thomas Tuchel alisema yeye na Mane walikubaliana "ilikuwa uamuzi bora zaidi kuhama".

"Tulikumbatiana kwa muda mrefu na sote tulikubaliana kuwa hatupendi kinachotokea sasa, lakini tunafikiri ni uamuzi bora zaidi katika hali hii," alisema kocha wa Bayern.

"Wakati mwingine mambo hayaendi jinsi kila mtu anavyotaka. Nimekuwa na uhusiano mzuri sana naye na hii itaendelea kusalia hivyo.

"Naweza kuelewa kabisa anahisi kuumia na pia singefurahi ikiwa mambo kama haya yangetokea.

"Ni wazi kwamba hatukuweza kutumia uwezo wote kamilifu, ambalo ni jukumu langu, lakini katika hali hii ilikuwa uamuzi bora zaidi kuondoka."

Al-Nassr walimsajili Ronaldo mshindi mara tano wa Ballon d'Or mwezi Desemba na wamefuata mtindo huo msimu huu kwa kuwaongeza kiungo wa kati wa Croatia Marcelo Brozovic, beki wa pembeni wa Brazil Alex Telles na kiungo wa kati wa Ivory Coast Seko Fofana.