Timu za taifa za raga za wachezaji saba kila upande kwa wasichana na wanaume zimepata ufadhili wa shilingi milioni 90 kwa miaka miwli kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kupitia jukwaa lake la M-Pesa.
Safaricom itatoa udhamini kwa timu za Kenya Sevens na Kenya Lionesses ambapo jezi za timu hizo mbili zitakuwa na nembo ya M-Pesa. Kwa jezi za Kenya Lionesses, nembo ya M-Pesa itakuwa upande wa mbele wa jezi hiyo wakati jezi ya Kenya Sevens itakuwa na nembo ya kampuni hiyo upande wa nyuma. Nembo iyo pia itakuwa kwenye kaptura za timu zote mbili.
Ushirikiano baina ya shirikisho la raga nchini KRU na Safaricom unajiri wakati mashindano ya raga ya dunia ya HSBC SVNS msimu wa 2024/2025 yanang’oa nanga Novemba 30 hadi Desemba mosi katika msururu wa Dubai 7s kabla ya kumaliza mashindano katika mwaka huu kwenye msururu wa Cape Town nchini Afrika Kusini.
Kenya itawasilishwa na timu ya wanaume ambayo inasafiri Jumatatu tarehe 25 kuelekea Dubai. Timu hiyo ilifuzu kushiriki HSBC SVNS baada ya kupandishwa ngazi kutoka kwa Challenger Series pamoja na Uruguay.
Kikosi cha wachezaji 13 kilichotajwa na kocha Kelvin Wambua kitaondoka nchini Jumatatu na kitashiriki misururu hiyo miwili mwaka huu dhidi ya timu za Ufaransa, Argentina, New Zealand, Fiji, Australia, USA, Afrika Kusini, Uingereza, Uhispania na Uruguay.