
Mkufunzi mkuu wa Shabana FC, Peter Okidi alisherehekea ushindi muhimu dhidi ya klabu ya Talanta, uliotia nguvu azma yao ya kuwania taji la Ligi Kuu ya Kenya.
Okidi anaamini kwamba ushindi huo mnono wa 4-2 kwenye Uwanja wa Dandora siku ya Jumapili ulionyesha uwezo na ari yao ya kutinga ubingwa msimu huu.
"Ilikuwa mechi nzuri kwetu na nilifurahishwa na jinsi tulivyotumia vyema nafasi tulizotengeneza kwenye mechi," Okidi alisema.
"Huu ni ushindi wa kuongeza ari ambao unarejelea matarajio yetu ya ubingwa wetu wa kwanza kabisa wa KPL," akaongeza.
Kocha mkuu wa Talanta Jackline Juma alikubali kushindwa, akisema wapinzani wao walikuwa wamejipanga zaidi.
"Wapinzani wetu walionekana kujipanga zaidi kwenye mechi," Juma alisema.
"Hata hivyo, nimeridhishwa na juhudi tulizoweka kwenye mchezo dakika za lala salama," aliongeza.
Austin Odongo aliweka Shabana mbele dakika ya 24 baada ya kutumia vyema makosa ya walinzi wa Talanta kabla ya Brian Michira kufanya matokeo kuwa 2-0 kwa mkwaju wa penalti dakika nane baadaye.
Talanta walipata bao la kufuta machozi kupitia kwa Cyprian Mang'eni kabla ya muda wa mapumziko. Licha ya kuanza vyema kipindi cha pili, matumaini ya Talanta yalififia pale Odongo alipoifungia Shabana bao la tatu dakika ya 61.
Hassan Mohamed aliipa Talanta matumaini ya kurejea mchezoni alipofunga dakika ya 67, muda mfupi baada ya kutambulishwa, huku Michira akihakikisha Shabana ushindi kwa shuti kali dakika za lala salama.
Katika mechi nyingine, Bidco United ilijinasua kutoka kwa msururu wa matokeo hasi, na kupata ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Mathare United katika uwanja wa Kenyatta.