

Kocha mkuu wa Tusker Charles Okere anaamini wamejipanga kimkakati kutwaa taji msimu huu baada ya kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Kenya Jumapili.
Wanamvinyo hao wa Ruaraka waliimarisha matumaini ya ya kushinda taji lao la 12 kutokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya Nairobi City Stars kwenye uga wa Kenyatta mjini Machakos.
Dennis 'Decha' Wanjala alipachika mpira wavuni dakika ya tano na kuipa timu hiyo yenye maskani yake Ruaraka ushindi huo muhimu uliowasukuma hadi alama 51, mbili mbele ya washindani wao wa karibu, Kenya Police.
Akizungumuza baada ya mechi hiyo, Okere alisema kuwa hawajisikii kuwa na shinikizo licha ya ushindani mkubwa uliopo katika kinyang'anyiro hicho.
Akitafakari changamoto za msimu, Okere alionyesha hali ya utulivu na azma. "Imekuwa msimu mgumu kucheza mechi kadhaa bila ushindi lakini tuna furaha hatimaye tumeweza kupata pointi nyingi katika kipindi kigumu sana cha msimu," Okere alisema.
"Ushindani bado ni mkubwa na timu zote tatu za juu zina nafasi sawa kwenye ubingwa lakini tumedhamiria kupambana hadi mwisho," aliongeza.
Okere alisema alibaini kuimarika kwa utendakazi wa kikosi chake baada ya msururu wa matokeo hasi.
“Tulijieleza vyema katika mechi hiyo na ninawaomba wachezaji waendelee na kasi hiyo,” Okere alisema.
Kinyume chake, Nairobi City Stars ilikabiliwa na kipigo cha kutamausha. Kocha msaidizi Peter Opiyo alilalamikia kadi nyekundu iliyotolewa kwa Otieno Omondi dakika ya 54, ambayo aliamini ilivuruga mpango wao wa mchezo.
"Ilitubidi kurejea kwenye ubao wa kuchora na kupanga upya baada ya kadi nyekundu," Opiyo alisema. "Hali ilizidishwa na bao la mapema tulilofungwa kwenye mechi," aliongeza.
Opiyo alisema lengo lao la haraka ni kujinusuru kutoka kwa uwezekano wa kushushwa daraja na kuhifadhi hadhi yao katika daraja la juu msimu ujao.