Faith Kipyegon ameshindwa katika jaribio lake la kuwa mwanamke wa kwanza katika historia kukimbia umbali wa maili kwa muda wa chini ya dakika nne.
Kipyegon, 31, alikimbia kwa muda wa dakika 4:06.42 kwenye uwanja wa Stade Charlety jijini Paris akilenga kufanikisha lengo hilo la kihistoria.

Muda huo ni sekunde 1.22 haraka zaidi kuliko rekodi yake ya dunia. Kipyegon alivaa vazi maalum la aerodynamic (skinsuit) na viatu vya kipekee, akilenga kukamilisha mizunguko ya chini ya sekunde 60 — sawa na kasi ya takribani kilomita 24 kwa saa.
Alipomaliza mzunguko wa tatu muda wake ulikuwa dakika 3:01.84, lakini matumaini ya kuvunja dakika nne yalianza kufifia katika mita 400 za mwisho.

Hata hivyo, alikamilisha mbio hizo kwa muda wa haraka zaidi katika historia kwa mwanamke kabla ya kuanguka ardhini kwa uchovu.
Utepe wa kumalizia mbio hizo ulishikiliwa na rafiki yake wa karibu na mwenza wake wa mazoezi, Eliud Kipchoge, ambaye mwaka 2019 alikua mtu wa kwanza duniani kukimbia marathon kwa muda wa chini ya saa mbili.
“Nimeonyesha kwamba jambo hili linawezekana, ni suala la muda tu. Kama si mimi, basi itakuwa mtu mwingine,” alisema Kipyegon.
“Sijakata tamaa, bado nitalifuatilia. Natumaini nitalifikia siku moja.