
Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia FC, wamefukuza benchi zima la ufundi baada ya kumaliza msimu bila kushinda taji lolote.
Hatua hiyo imejiri siku chache tu baada ya kocha mkuu Zedekiah Otieno 'Zico' kulazimika kujificha kutoka kwa mashabiki wenye hasira katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex kufuatia kichapo cha 2-1 dhidi ya Nairobi United kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Kenya (FKF Cup).
Mabingwa hao mara 21 wa Ligi Kuu ya Kenya pia walipoteza taji lao kwa Kenya Police baada ya kumaliza msimu katika nafasi ya pili.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier, alisema kuwa wamefikia uamuzi mgumu wa kuachana na benchi lote la ufundi pamoja na wanachama wa kikosi cha usalama.
“Gor Mahia Football Club inapenda kuwafahamisha mashabiki wake, wadau, na umma kwa ujumla kwamba imekubaliana kwa pamoja na benchi lote la ufundi, wakiwemo wanachama wa kikosi cha usalama, kuachana rasmi kuanzia tarehe 2 Julai 2025,” alisema Rachier.
“Uamuzi huu unafuatia tathmini ya kina ya ndani na ni sehemu ya mchakato mpana wa mageuzi unaolenga kuimarisha uwezo wa kiufundi na kiutendaji wa klabu kuelekea msimu wa 2025/26.”
“Kuachana huku kumefikiwa kwa makubaliano ya amani na kwa nia njema, huku klabu ikitambua na kuthamini mchango wa wahusika waliotoka. Tunawashukuru sana kwa kujitolea, weledi, na huduma yao kwa klabu katika kipindi cha uongozi wao,” aliongeza.
Rachier aliwahakikishia mashabiki waaminifu wa timu hiyo kuwa juhudi zote zitafanyika kurejesha hadhi ya Gor Mahia.
“Tunapoanza ukurasa mpya, Gor Mahia FC inasalia kuwa na dhamira ya kujenga msingi imara wa mafanikio ya ushindani ndani na nje ya uwanja. Taarifa zaidi kuhusu mabadiliko ya benchi jipya la ufundi zitatolewa hivi karibuni.”