
London, Uingereza, July 23, 2025 — Winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho, ameachwa nje ya kikosi cha wachezaji 32 watakaosafiri kuelekea Marekani kwa ziara ya maandalizi ya msimu mpya, ishara kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 yuko mbioni kuondoka Old Trafford msimu huu wa joto.
Garnacho hajakuwa sehemu ya mipango ya kocha Ruben Amorim tangu United walipopoteza fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham mwezi Mei.
Tangu wakati huo, aliwekwa benchi katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa baada ya kuchapisha ujumbe unaoaminika kumkosoa kocha wake kwenye mitandao ya kijamii.

Chelsea Yapewa Nafasi Kubwa ya Kumsajili
Chelsea wamekuwa wakimvizia Garnacho tangu dirisha la Januari, lakini walijiondoa awali kutokana na bei ya pauni milioni 70 waliyowekewa na United.
Hata hivyo, taarifa kutoka ESPN zinaeleza kuwa United sasa wako tayari kumuuza kwa pauni milioni 40 ili kupata fedha za kuwasajili wachezaji wapya.
“Garnacho angependa kubaki kwenye Ligi Kuu na kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya,” chanzo cha karibu na mchezaji huyo kiliiambia ESPN. “Chelsea ni chaguo la kuvutia kwake.”
Klabu ya Napoli pia imeonesha nia ya kumsajili, lakini Garnacho anaonekana kupendelea kusalia Uingereza.
Manchester United Yasaka Fedha kwa Mauzo
Manchester United tayari imewasajili Matheus Cunha na Bryan Mbeumo katika dirisha hili la usajili, na sasa wanahitaji kuuza baadhi ya wachezaji ili kuendelea na mipango yao sokoni.
“Garnacho ana kipaji kikubwa lakini haimo kwenye mipango ya Amorim,” alisema afisa wa klabu. “Huu ndio wakati sahihi wa kumuuza.”
Mbali na Garnacho, Jadon Sancho — aliyewahi kuchezea Chelsea — pia ameachwa kwenye kikosi cha Marekani, huku hatima yake pia ikiwa njia panda.
Ujumbe wa Mitandao Wazua Taharuki
Garnacho ameongeza moto kwenye uvumi wa uhamisho wake kwa kupakia video ya mazoezi kwenye ukurasa wake wa Instagram, video yake ya kwanza kwa wiki tatu, ikimuonesha akijifua gym huku sauti ya nyuma ikisema: “Huu ndio siri yangu… hakuna siri — ni bidii tu na kujitolea.”
Akaandika kwa kifupi: “Najitayarisha…”
Wakati hatma yake ikiwa bado haijathibitishwa rasmi, kila dalili zinaonesha Garnacho anaelekea kuondoka Old Trafford — na Chelsea iko tayari kumchukua.