
NAIROBI, KENYA, Agosti 3, 2025 — Kiungo wa Harambee Stars na Gor Mahia, Alpha Onyango, ametajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi katika ushindi wa 1-0 dhidi ya DR Congo kwenye mechi ya ufunguzi wa Kundi A ya CHAN 2024.
Onyango, ambaye alionyesha mchezo wa kiwango cha juu katika kiungo cha kati, alisema ni fahari kubwa kuvalia jezi ya taifa na kuchangia ushindi muhimu kwa timu ya Kenya.
“Nimeheshimiwa sana kuteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi katika pambano letu la CHAN dhidi ya DR Congo. Najivunia kuivaa beji hii na kujitolea kwa ajili ya timu. Ushindi huu ni kwa ajili ya Kenya. Tunasonga mbele!” aliandika Onyango kupitia mitandao ya kijamii.
Ushindi wa Kihistoria
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani ilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa soka, akiwemo Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Bao pekee la Austin Odhiambo lilitosha kuhakikisha Kenya inaanza kampeni yake ya CHAN kwa ushindi wa maana.
Rais Ruto, ambaye aliwashangaza wachezaji kwa kuwa tembelea chumba cha kubadilishia baada ya mechi, aliahidi kuwazawadia wachezaji Shilingi milioni moja kila mmoja kwa ushindi huo.
Onyango Asifiwa
Uchezaji wa Alpha Onyango uligonga vichwa vya habari, huku wachambuzi wa soka na mashabiki wakimsifu kwa nidhamu ya juu, uwezo wa kudhibiti mchezo, na ushawishi mkubwa uwanjani.
Mwanzo wa Ndoto
CHAN 2024 ni mashindano ya wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani pekee, na Onyango amekuwa mfano bora wa mafanikio ya vipaji vya humu nchini.
Kwa wachezaji kama Onyango, mashindano haya ni jukwaa la kujionyesha na kufungua milango ya taaluma za kimataifa.
“Hii ni nafasi ya kipekee kwa sisi wachezaji wa ligi ya ndani. Tunajua macho yote yako kwetu, na hatutaki kuangusha taifa,” alisema Onyango baada ya mechi.
Kenya Yashika Usukani
Kwa ushindi huu, Harambee Stars sasa wako kileleni mwa Kundi A na wanatarajiwa kukutana na Angola katika mechi ijayo. Mafanikio hayo yametoa motisha mpya kwa kikosi hicho, ambacho kwa mara ya kwanza kinashiriki CHAN kama mwenyeji.
FKF na serikali wameonyesha mshikamano mkubwa na timu hiyo, huku ahadi ya marupurupu ikitolewa ili kuwapa wachezaji motisha zaidi.
“Tuna imani na vijana hawa. Tumewawekea mazingira bora, sasa ni wakati wao kutuletea fahari,” alisema Rais Ruto.